Habari Picha

Shirika la “Ni Hekima Pekee” kupambana na mimba za utotoni

on

Judith Ferdinand, BMG Habari

Mkurugenzi wa Shirika la Ni Hekima Pekee, Onesmo Kajuna amesema miongoni mwa changamoto zinazosababisha changamoto ya mabinti kupata mimba katika umri mdogo ni ukosefu wa mawasiliano baina ya watoto, wazazi pamoja na wanajamii kwa ujumla.

Kajuna anasema kwa kulitambua hilo shirika la Ni Hekima Pekee limeanzisha na mradi wa Wasiliana unaolenga kuwasaidia wasichana wanaotoka katika mazingira hatarishi katika Kata ya Lwanhima Jijini Mwanza.

Alisema mradi huo una lengo la kusaidia wasichana hao wasiweze kupata mimba katika umri mdogo na kuzaa watoto ambao wataendelea kutoka kwenye mazingira magumu kwa  kuwapa elimu ya kujitambua na namna ya kujikimu kwa kufundishwa stadi mbalimbali za maisha.

Aidha alisema shirika liko mbioni kuanzisha darasa la ushonaji/ ufumaji wa vitu mbalimbali ambavyo vitawasaidia kujikomboa kiuchumi kwa waliopo  mtaani na walioshuleni watapatiwa elimu ya uzazi,usafi,lishe na madhara yatokanayo na madawa ya kulevya.

Hata hivyo alisema jamii iendelee kuelimishwa kwa njia mbadala ambayo itaweza kuwafikia kwa  kiwango kikubwa,kuwepo kwa mabaraza ya kata ambayo yatatumika kama jukwaa la mabinti kuweza kubadilisha mawazo,kujadili,kujifunza na kuelimishana juu ya masuala yanayowahusu.

“Inatakiwa kuwa na vipindi vya elimu ya mabinti kujitambua hasa shuleni pamoja na kuwa na mabaraza ya kata ambayo yatakuwa kama majukwaa ya kusemea wasichana na kuwawezesha kuwa mabalozi kwa wenzao”. Alisema Kajuna.

Kwa upande wake Mratibu wa shirika hilo, Getruda Edward alisema wamewafikia wasichana ambao hawapo shuleni 48 na waliopo shule  za msingi 144 wenye umri kati ya miaka 12 na 18 na kuwafundisha kujitambua na kujiamini.

Edward alisema wasichana hao wanapewa elimu ya kutokubali kufanya mapenzi kabla ya wakati kwa waliopo shuleni na waliopo nyumbani huku waliojifungua wakielimishwa ili wasipate tena mimba.

Recommended for you