Habari Picha

Shirika la Nihekima Pekee lakabidha mahitaji kwa wanafunzi Jijini Mwanza

on

Judith Ferdinand, BMG Habari

Wazazi na walezi mkoani Mwanza wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuwahimiza watoto wao kutambua umuhimu wa elimu.

Mkurugenzi wa shirika la Nihekima Pekee, Onesmo Kajuna ametoa rai hiyo wakati akikabidhi msaada wa vifaa vya shule kwa wanafunzi 40 wa shule ya msingi Sahwa iliyopo Kata ya Lwanhima Jijini Mwanza.

Kajuna alisema vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni mbili na laki tano, vitasaidia wanafunzi hao kuendelea na masomo kwani wakati mwingine wanakatisha masomo kutokana na familia wanazotoka kutokuwa na uwezo wa kuwahudumia na hivyo kuwa chanzo cha kuyumba kimasomo.

“Hii Kata ina uhitaji na inakabiliwa na changamoto ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu kuanzia ngazi ya familia, hivyo tumewapa msaada wa vifaa mbalimbali vya shule  ikiwemo madaftari, karamu, viatu, sare za shule pamoja na mifuko ya kuhifadhia madaftari”Alisema Kajuna.

Naye Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Lwanhima, Enock Henry alisema wakati huu ni wakutambua umuhimu wa elimu hivyo wazazi wanapaswa kutoa kipaumbele kwa watoto wao kwani ni haki yao ya msingi.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Sahwa, Mayobyo Mazigo aliwataka wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao kwa ukaribu na kuacha kuwatumikishwa kazi za nyumbani watoto wao katika muda wa shule.

Misoji Mungu ambaye ni mmoja wa wazazi  wa watoto walionufaika na msaada huo alisema changamoto kubwa inayowakabili ni tabia ya watoto kutoka nyumbani wakiaga wanaenda shule kumbe hawafiki na badala yake kwenda kushinda kwenye mlima hadi wenzao wanapotoka shuleni na kujumuika nao kurejea nyumbani.

Shirika la Nihekima Pekee lifanya kazi ya kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Mwanza. Soma zaidi HAPA

Recommended for you