Habari Picha

Mwenyekiti wa UVCCM Taifa awapa somo wahitimu wa vyuo vikuu

on

Judith Ferdinand, BMG

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Kheri James amewahimiza vijana wa vyuo vikuu nchini kuwa wabunifu na kuitumia vyema elimu yao kutengeneza ajira badala ya kutegemea kuajiriwa.

James aliyasema hayo jana Jijini Mwanza kwenye Mahafali ya Shirikisho la Vyuo Vikuu Tanzania, Mkoa wa Mwanza, ambapo aliwapa changamoto wahitimu hao hususani vijana kuwa na sababu za wao kutaka kuajiriwa badala ya kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao.

Alisema baadhi ya vijana na wasomi nchini wamekuwa wakilalamika kuhusu suala la ukosefu wa ajira bila wao kuionyesha jamii ubunifu walionao kwa kujitolea kufanya shughuli mbalimbali zinazoweza kuwashawishi waajiri kuwaajiri.

“Hauwezi tu kuajiriwa kwa sababu tu umesoma, unatakiwa uwe na sifa ya ziada ikiwemo kujitolea katika shughuli mbalimbali, kuleta mabadiliko chanya katika jamii kupitia elimu uliyonayo, heshima, uvumilivu na nidhamu na hapo utakuwa umeipa sababu jamii kwanini uajiriwe”. Alisema James.

Aliwahimiza vijana kutumia elimu zao katika kuanzisha miradi mbalimbali itakayowapa ajira na kuwaajiri wengine huku serikali ikitumia nafasi hiyo kuwaunga mkono “kwani lifti inamkuta mtu barabarani na siyo nyumbani”.

Kwa upande wake Katibu wa Shirikisho la Vyuo na Vyuo Vikuu Tanzania (SENETI) mkoani Mwanza, Seleman Baruani alisema shirikisho hilo lina jumla ya matawi (vyuo) 30 kwa mkoa wote na kwamba wanakabiliwa na changamoto ya mikopo na upigaji faini wanafunzi wanaochelewa kulipa ada kwa wakati hasa vyuo binafsi pamoja na mikopo ya kufanyia ujasiriamali.

Alisema shirikisho limeandaa mkakati wa kuanzisha miradi ya ufugaji samaki, kuku, bata, mbuzi, ng’ombe, kilimo cha mbogamboga pamoja na karakana ya ufundi ili kufikia uchumi wa viwanda, ambapo alimuomba Katibu James kuwasaidia kupata eneo la hekali 30 kwa ajili ya kufanyia shughuli hizo.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Mwanza, Jonas Lufungulo alisema changamoto zipo katika maisha hivyo ni wakati mwafaka kwa wahitimu hao kupambana nazo ili kuleta mabadiliko na maendeleo katika jamii ambapo wanatakiwa kuwa wavumilivu ili kufikia ndoto zao.

Hata hivyo Katibu wa UVCCM Mkoa wa Mwanza, Odilia Batimayo alisema vijana wa vyuo waendelee kushirikiana na chama kwa vile wao ni wasomi watumie elimu yao katika kusaidia jamii huku akiwasihi kutumia vyema mitandao ya kijamii badala ya kuandika mambo maovu.

Mwenyekiti UVCCM Taifa, Kheri James (wa tatu waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali

Mmoja wa wahitimu akipokea cheti

Recommended for you