Habari Picha

Tuzo ya heshima kwa Waziri wa Kilimo Tanzania

on

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa (kulia) akimkabidhi tuzo ya heshima Waziri wa Kilimo Mhe.Dkt Charles Tizeba kwa kuimarisha sekta ya Ushirika nchini. Ni katika kilele cha Siku ya Ushirika Duniani 2018 iliyofanyika kitaifa uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza jana Julai 07, 2018.

Na Mathias Canal-WK, Mwanza

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amemkabidhi tuzo ya heshima Waziri wa Kilimo Mhe.Dkt Charles Tizeba kwa kazi kubwa aliyoifanya na anayoendelea kuifanya katika kuimarisha sekta ya ushirika nchini.

Tuzo hiyo ilitolewa jana kwenye kilele cha Siku ya Ushirika Duniani kwa niaba ya wanaushirika walioandaa tuzo hiyo ikiwa ni heshima na utumishi mkubwa kwa Waziri Tizeba katika kipindi kifupi alichotumikia wizara hiyo na kurudisha imani ya ushirika kwa wananchi.

Tuzo hiyo kwa Dkt Tizeba ilitolewa wakati ikiwa ni siku moja pekee imepita tangu waziri huyo atangaze kiama kwa viongozi na baadhi ya watendaji wa vyama vya ushirika wanaofanya ubadhilifu wa mali za wanaushirika kwa manufaa yao pekee pasina kuwanufaisha wanachama wote.

Juzi Mhe. Dkt Tizeba alieleza kwa ukali kuhusu ubadhilifu wa rasilimali za ushirika unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika kwenye hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la wanaushirika Tanzania katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza.

Kongamano hilo liliambatana na maonesho ya bidhaa na shughuli zinazofanywa na vyama hivyo vya ushirika kote nchini ambapo wanachama walipata fursa ya kubadilishana uzoefu na kujadili mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo katika uendeshaji wa sekta ya ushirika nchini na kutoa maoni yao kwa serikali.

Dkt.Tizeba alisisitiza kuwa serikali inafanya juhudi mahususi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanahamasishwa na hatimae kujiunga kwenye vyama vya ushirika kulingana na shughuli zao za kiuchumi ili kuondoa dhana kuwa vyama vya ushirika ni kwa ajili ya Kilimo cha Mazao ya biashara ya nchi za nje.

Pia alisema kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM kupitia serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini mchango wa ushirika wa Taifa katika kuyafikia malengo ya milenia na malengo mbalimbali ya nchi kama uimarishwaji wa sekta ya viwanda, Kilimo, Mifugo, uvuvi na biashara na kuchangia katika ongezeko la kipato kwa wananchi na hatimaye kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.

Tuzo hiyo ya kuimarisha sekta ya ushirika nchini pia ilitolewa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim M. Majaliwa.

Waziri wa Kilimo Mhe.Dkt Charles Tizeba akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani

Baadhi ya wananchi na wanaushirika kutoka vyama mbalimbali waliohudhuria maadhimisho hayo

Wazori Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa (kulia) akisalimiana na Waziri wa Kilimo Mhe.Dkt Charles Tizeba baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Mwanza

Recommended for you