Audio & Video

TAASISI YA COYETA YAZINDUA MAABARA YA KISASA JIJINI MWANZA

on

Taasisi ya elimu ya watu wazima, College Of Youth In Tanzania COYETA imezindua maabara mpya na ya kisasa Jijini Mwanza, kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wake kusoma na kujifunza kwa vitendo zaidi.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, mgeni rasmi Askofu Dkt. Elias Simon Ndaki ambaye ni Askofu Mkuu wa Kanisa la FPCT Jimbo la Mwanza, ameipongeza taasisi hiyo kwa kuanzisha maabara hiyo ambayo itawawezesha wanafunzi kupata elimu bora.

“Elimu inapokuwa ya vitendo zaidi inamjengea mtu uwezo hivyo itumieni vyema maabara hii katika kufanya mambo mazuri. Pia lazima tuwekeze kwenye elimu ambayo mtu akiikamata itamsaidia”. Amesema Askofu Ndani huku akiusihi uongozi wa taasisi hiyo pia kujikita kwenye ujenzi wa mabweni ili kutatua kabisa changamoto hiyo kwa wanafunzi.

Akiwasilisha mada kwenye uzinduzi huo, Mchungaji Innocent Makaza wa kanisa la FPCT Mjini Kati Jijini Mwanza, amesisitiza juu ya umuhimu wa elimu ya kiroho na elimu dunia, akisema kwamba kupitia elimu ni rahisi mwanadamu kufikia mafanikio yake.

Mwenyekiti wa bodi ya taasisi hiyo ya COYETA, Nzalila Godfrey amesema mikakati yake ya miaka mitano ijayo ni pamoja na kutoa mafunzo ya elimu kwa ngazi ya cheti hadi stashahada, kujenga mabweni kwa ajili ya wanafunzi na pia kuwa taasisi inayoongoza Kanda ya Ziwa kwa kutoa elimu bora.

Baadhi ya wanafunzi wa taasisi hiyo inayomilikiwa na Kanisa la FPCT, Tutu Maligo na Saimon Muniko, wamesema uwepo wa maabara hiyo ni fursa kubwa kwao kwani itawawezesha kujifunza kivitendo zaidi na hivyo kukuza kiwango chao cha ufaulu.

 

Taasisi ya COYETA iliyopo jengo la Vijana Centre Mlango Mmoja Jijini Mwanza, inatoa mafunzo mbalimbali ikiwemo elimu ya Uhasibu, Manunuzi na Ugavi, Biashara na Utawala, Elimu ya sekondari kwa miaka miwili, wanaorudia mitihani, Hoteli, Utalii, Kiingereza, Muziki na mengineyo.

TAZAMA VIDEO HAPO CHINI

Mgeni rasmi, Askofu Dkt. Elias Simon Ndaki ambaye ni Askofu Mkuu wa Kanisa la FPCT Jimbo la Mwanza akikata utepe kuashiria ufunguzi wa maabara hiyo

Mwenyekiti wa bodi ya taasisi hiyo ya COYETA, Nzalila Godfrey, akitoa ufafanuzi kuhusu maabara hiyo

Baadhi ya wanafunzi wa COYETA wa wakishuhudia maabara iliyozinduliwa leo

Mgeni rasmi, Askofu Dkt. Elias Simon Ndaki ambaye ni Askofu Mkuu wa Kanisa la FPCT Jimbo la Mwanza

Mchungaji Innocent Makaza wa kanisa la FPCT Mjini Kati Jijini Mwanza, akiwasilisha mada

Mwenyekiti wa bodi ya taasisi hiyo ya COYETA, Nzalila Godfrey, akiwasilisha taarifa ya taasisi hiyo

Baadhi ya wanafunzi na watumishi wa COYETA

Baadhi ya wanafunzi na watumishi wa COYETA

Wageni waalikwa

Waimbaji wa Injili Jijini Mwanza

BMG Habari, Pamoja Daima!

Recommended for you