Habari Picha

Kampuni ya Taxify kurahisisha huduma za usafiri Jijini Mwanza

on

Judith Ferdinand, BMG

Wakazi wa Jiji la Mwanza wanatarajia kunufaika kukua kwa sayansi na teknolojia inayochochea upatikanaji wa huduma ya usafiri wa haraka kwa njia ya kidijitali (mtandao).

Remmy Eseka ambaye Meneja Uendeshaji wa kampuni ya Taxify ambayo inahusika na utoaji huduma ya usafiri kwa njia ya kidijitali aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa huduma za kampuni hiyo Jijini Mwanza.

“Tulifanikiwa kupokea maombi mengi kutoka kwa wakazi wa Jiji la Mwanza waliokuwa na shauku ya kutumia huduma yetu ambapo madereva wameisha sajiliwa kwenye jukwaa letu na tayari tumeishaona safari zao na ninaamini Mwanza ipo tayari kwa huduma ya usafiri kwa njia ya mtandao”. Alisema Eseka.

Alisema Taxify inaunganisha watumiaji na watoa huduma ya usafiri ulimwenguni kote katika kurahisisha huduma hiyo kwa haraka na ufanisi huku teknolojia ya biashara yake ikiwanufaisha wote madereva ambao wanalipwa kamisheni na abiria wanalipa nauli ya gharama nafuu.

Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Mary Tesha ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa Mwanza John Mongella alisema katika miji iliyoendelea majukwaa ya usafirishaji kwa njia ya mtandao yanaonekana kupunguza msongamano wa magari mijini, kuongeza ajira, kupunguza uchafu wa mazingira na kuboresha maisha ya wakazi wa maeneo hayo hivyo historia imeandikwa kwa Jiji la Mwanza kuwa kwenye ramani ya majiji yaliyoendelea kwa kutumia huduma ya Taxify.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Taxi mkoani, Mwanza Beatus Milambo alisema wameipokea Taxify kwani wanaamini watafanya kazi katika mfumo mzuri na watapata wateja kwa urahisi japo madereva wanakabiliwa changamoto ya kuwa na simu zisizokuwa na uwezo wa kuingia kwenye mtandao (intaneti).

Kupitia huduma ya Taxify, mteja ataweza kupata huduma ya usafiri wa “tax” kwa gharama nafuu ambapo huduma hiyo inawezeshwa na mtandao wa intaneti pindi mteja anapohitaji huduma ya usafiri katika eneo alilopo.

Recommended for you