Audio & Video

TBS yawasaidia wajasiriamali ili kukuza uchumi wa viwanda

on

Judith Ferdinand, BMG

Ili kusaidia kukua kwa viwanda vidogo nchini, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeweka utaratibu wa kugharamia wajasiriamali kupata leseni ya nembo ya ubora huku kigezo kikubwa kikiwa ni mjasiriamali kuwa na cheti kutoka shirika la viwanda vidogo SIDO.

Akizungumza katika semina ya wajasiriamali wadogo mkoani Mwanza, Kaimu Mkuu wa Ofisi ya TBS  Kanda ya Ziwa Joseph Makene alisema nembo hiyo itatumika kwa miaka mitatu bila malipo na baadae mjasiriamli ataanza kuchangia mwaka wa nne robo ya gharama la leseni, mwaka wa tano nusu, wa sita robo tatu na wa saba atalipa gharama kamili.

Makene aliwataka wajasiriamali kufuata taratibu za kupata nembo ya ubora ambayo itasaidia bidhaa zao kushindana vizuri katika soko la ndani na nje ya nchi na kuwataka kuacha tabia ya kughushi nembo au biashara ya mwingine kwani hatua za kisheria zitachukuliwa.

Alisema faida za uwekaji nembo ya ubora  humpa uwezo wa kushindana sokoni,humuondolea usumbufu wa kupima bidhaa kwa kuzingatia matakwa ya mnunuzi,humkinga dhidi ya ushindani wa bidhaa sokoni zisizokuwa na ubora,humthibitishia mlaji kuwa bidhaa husika inafaa kwa matumizi,humuhakikishia usalama kiafya na hulinda mazingira.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora TBS Nickonia Mwambene alisema, lengo la semina hiyo, ni kumpatia mjasiriamali elimu bora juu ya kuzalisha bidhaa zenye ubora na umuhimu wa kuweka nembo ya ubora ili kufikia uchumi wa kati kwani wao ndio msingi wa kupata viwanda vya kati.

Mwambene alisema,kwa kuzingatia hilo serikali ikaona wananchi wafuatwe kwenye maeneo yao wapatiwe elimu ili waweze kutengeneza bidhaa zenye kiwango,salama iliyothibitishwa na yenye nembo ya ubora ambayo itaweza kipita mipakani bila usumbufu na kuweza kushindana katika soko la Afrika  Mashariki.

Alisema kupitia semina hiyo, wajasiriamali wataweza kukidhi vigezo vya ubora na hivyo kupata fursa ya kimasoko ndani na nje ya nchi ikiwemo Kenya pia aliwataka washiriki  kuzingatia na kufanyia kazi waliofundishwa kwa faida ya taifa na ambapo hawajaelewa waulize katika Ofisi za TBS.

Afisa Biashara  mkoa  wa Mwanza, Yessaya Sikindene aliwataka, wajasiriamali waendelee kuzalisha bidhaa zenye ubora ambayo watapeleka katika maonyesho ya nane nane yanayotarajia kuanza Augosti 1-8 mwaka juu katika viwanja vya Nyamongoro.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo  Erenest Hillu alisema, semina hiyo itawasaidia kuondokana na changamoto  zilizokuwa zikiwakabiri ikiwemo ya vifungashio, na wametambua  umuhimu wa kusajili na nembo ya ubora katika bidhaa zao namna zinavyoweza kusaidia katika ushindani wa soko hivyo wanatarajia kuendelea kuzalisha bidhaa zenye kiwango na bora nchini.

SOMA Wajasiriamali mkoani Mwanza wapatiwa semina na TBS 

Recommended for you