Habari Picha

TCCIA yaahidi mazingira bora ya uwekezaji kwa Waturuki

on

Washiriki wa Turkish Exporters Week kutoka Tanzania wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Na Edwin  Soko, Istanbul Uturuki

Chama cha wafanya bishara, viwanda na kilimo Tanzania  (TCCIA), kimewaahidi wawekezaji  toka  Uturuki kuwa kitasaidia   kuweka  mazingira  mazuri  ya  uwekezaji ili  waweze  kudumisha   ushirikiano wa  kibiashara  kati  ya  Tanzania  na  Uturuki.

Hayo  yamesemwa na  Rais wa TCCIA, Bwana Octavian  Mshiu wakati wa majadiliano  ya  pamoja  kati  ya  wafanyabiashara wa  Nchi za   Kiafrika na    viongozi  wa juu toka Mamlaka  za biashara  na  uchumi  Nchini  Uturuki.

Mshiu alisema, TCCIA  wana  mipango  ya  muda  mfupi  na mrefu  kwenye  kuhakikisha  uendelezaji wa biashara  unakuwepo    kati  ya   Nchi  hizo  mbili  ili  kutimiza  azma ya  Serikali  ya  Tano  ya  kuhimiza  uchumi wa  viwanda  na  hivyo  kufikia  uchumi wa kati ifikapo  mwaka  2030.

Pia  alisema  kuwa,  TCCIA  wana wajibu wa kufanya  hivyo  ili  kuhakikisha  wawekezaji  wengi  wa  nje  wanatambua fursa za uwekezaji  zilizopo  Nchini, ambazo  pia  zinaweza kuchochea   ushirikiano wa  wafanya bishara  wa Tanzania na wale wa nje.

“Nchi  ya  Uturuki  imeendelea  kwenye   teknolojia  kiasi  cha  kuwa na wataalamu wengi  katika  Nyanja    hiyo,  hivyo  tukishirikiana  nayo   Tanzania  tunaweza  kujenga  viwanda   vingi  hasa   vidogo  na kati  ili    kutoa  ajira  kwa watanzania  wengi na  kukuza  uchumi wa Nchi” Alisema  Mshiu.

Pia  Mwenyekiti wa  TCCIA  diaspora  ya  Uturuki bwana  Jumanne  Miraji  Simba  alisema kuwa, uwepo wa  TCCIA  Nchini  na TCCIA Uturuki  Diaspora, utasaidia  kuunganisha    mahusiano  mapana  ya  kibiashara  baina  ya  Nchi  hizo  mbili, na kukuza   uchumi kuanzia  kwa  mwananchi  mmoja  mmoja  hadi  Taifa.

“Sisi  pia  tunajivunia kuwa  na  viongozi  hodari  wa TCCIA  Nyumbani , ambao  kimsingi wamekuwa  wakitujenga  sana  na kutufanya  kushiriki kikamlifu  kwenye  kutafuta   fursa  za  uwekezaji  kwa kuwaunganisha  Wafanyabiashara  wa  hapa   Uturuki na  Tanzania” Alisema  Simba.

Naye  Balozi wa  Tanzania  Elizebert   Kihondo    wakati  akikutana  na  wafanyabiashara  wa Tanzania hakusita  kuwapongeza  viongozi  wa TCCIA  kwa kuchukua   jukumu kubwa  la  kuandaa  mazingira  mazuri  ya  uwekezaji  ili  wawekezaji wanapofika  kuwekeza  Nchini  wakute  mazingira  safi  na  salama  ya  uwekezaji.

Pia  alieleza kuwa  Serikali  itaendelea kuwa na  sera  pamoja  na  sheria  nzuri  zenye  kuwavutia  wawekezaji   kuwekeza  Tanzania.

Wafanyabishara  zaidi  ya  ishirini  na  sita  wa Tanzania  walishiriki  kwenye  kongamano  la  kiuchumi  lijulikanalo  kwa  jina  la  Turkish   Exporters   Assembly   Week  katika  ukumbi wa   Istanbul Congress    Center, mji  wa istabul  Uturuki, kwa  siku  tatu kuanzia  Oktoba  1 –  3 mwaka  huu.

Makamu wa Rais wa TCCA, Octavian Mshiu akiwa kwenye maandalizi ya mkutano wa Turkish Exporters Assembly Week nchini humo.

 

Recommended for you