Michezo

TIMU MPYA YA SOKA YAZINDULIWA JIJINI MWANZA

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Timu ya soka Black Lion SC ya Jijini Mwanza inayoshiriki ligi daraja la nne wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, imewaomba mashabiki wake kujitokeza kuwasapoti kwa kuwachangia fedha ili waendelee kufanya vyema katika mechi zao zilizosalia kufikia lengo la kupanda daraja la  tatu ngazi ya mkoa huo.

Timu hiyo ni miongoni mwa timu tisa zilizofuzu kucheza hatua ya mtoano (tisa bora) katika Ligi daraja la nne wilaya ya Nyamagana, ikiwa imecheza michezo saba na kujikusanyia pointi 21 bila kupoteza mchezo, hatua ya mtoano ya ligi hiyo inatarajiwa kuanza Agosti 14, mwaka huu.

Akizungumza na wakati wa uzinduzi wa timu hiyo uliofanyika jijini hapa, Msemaji wa  timu hiyo, Mohamedi Selemani alisema wanalenga kufikia mbali zaidi kwa kufanya vizuri katika ligi hiyo na kufuzu ligi daraja la tatu Mkoa wa Mwanza na hatimaye kucheza Ligi kuu Tanzania.

“Timu hii  inashiriki ligi daraja la nne ngazi ya wilaya  tumecheza  mechi saba hatujapoteza hata moja hadi hivi sasa tuna pointi 21 lengo ni  kuendelea kutembeza bakora kwa wapinzani wetu ili tuweze kuchukua ubingwa wa wilaya.

Pia alisema kutokana na  juhudi  za  wachezaji  wameamua kufanya  uzinduzi  wa  timu  yao, ili itambulike  rasmi  kwani wameshiriki mabonanza mbalimbali lengo ni kurudisha heshima ya soka jijini hapa.

Aliongeza kuwa, kikosi chao chenye wachezaji chipukizi 25 wote wametokana na falsafa yao ya kuibua vipaji kwa vijana kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya  jiji hilo,  kwani michezo ni ajira  kama ilivyo kazi nyingine sambamba na hilo amewaomba wadau na mashabiki mbalimbali  kuipiga tafu  kwa kutoa michango yao ya hali na mali ili kuisaidia kusonga mbele katika soka.

“Nawaomba   wadau  na mashabiki mbalimbali wa soka  kutushika mkono kwani timu hii haina  mtu wa kuisaidia  na inakabiliwa na changamoto mbalimbali, sanjari na hilo  nawaomba wazazi wenye vijana wenye vipaji kuwaleta kwani kituo hiki kina lengo la kuchukua wachezaji  zaidi ya 100,” alisema.

Hata   hivyo aliwataka wachezaji  kujitambua, kujithamini,  kuwa na heshima  na kuipenda kazi yao, ili kuweza kufanya vizuri katika mechi mbalimbali zinazoendelea  sambamba na kufuata maelekezo kutoka kwa viongozi wa timu hiyo.

Recommended for you