Michezo

Timu ya Alliance FC yabanwa Jijini Mwanza

on

Judith Ferdinand, Mwanza
Timu ya Alliance FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza Tanzania Bara imeshindwa kufurukuta dhidi ya timu ya Phantom FC inayotarajia kushiriki ligi daraja la tatu mkoa wa Mwanza.

Katika mchezo wa kirafiki uliotimua vumbi juzi katika uwanja wa Butimba Jijini Mwanza, timu hizo zilitoka suluhu ya bao 2-2 ambapo mchezo huo ulikuwa maalumu kwa ajili ya timu zote kujiandaa na ligi husika.

Kipindi cha kwanza dakika ya 20 timu ya Phantom FC ilipata goli kwa mkwaju wa penati kupitia Samweli Jackson baada ya mchezaji wao Daniel Chintu kufanyiwa madhambi huku kipindi cha pili dakika ya 62 Alliance FC wakisawazisha goli kupitia Zabona Hamisi.

Hata hivyo dakika ya 83 mshambuliaji wa Phantom FC Deogratius Simon aliongeza goli pili huku Alliance FC wakipata goli la kusawazisha dakika ya 86 kwa njia ya mkwaju wa penati tena kupitia Bruno John baada ya Suma Makoroso kufanyiwa madhambi na hivyo hadi mpira unamalizika matokeo yalikuwa 2-2.

Kocha Msaidizi wa Alliance FC, Kessy Mziray alisema mchezo ulikuwa mzuri ingawa kulikuwa na mapungufu ambayo kama benchi la ufundi atayafanyia kazi ili kujiweka sawa kuelekea kwenye mchezo wao na Biashara ya Musoma.

Mziray alisema wametumia mchezo huo kwa ajili ya kuandaa kikosi kitakachocheza na timu ya Biashara FC ya Mkoani Mara baada ya wachezaji wake wanne kupewa kadi nyekundu katika mchezo wao na Dodoma FC uliopigwa mwishoni mwa mwaka jana.

Mziray alisema Phantom FC ni  timu nzuri na ana imani itafanya vizuri kwenye ligi daraja la tatu mkoani Mwanza.

Mwenyekiti wa Mashindano wa timu ya Alliance FC, Yusuph Budodi alisema maandalizi yapo vizuri na wamejiandaa na mchezo dhidi ya Biashara FC na kwamba muda wowote timu hiyo itaweka kambi maeneo ya karibu na Musoma.

Budodi alisema mchezo huo kwao ni muhimu ili wapate pointi tatu zitakazosaidia kupanda ligi kuu hivyo aliomba waamuzi kuchezesha mpira kwa kufuata sheria 17 za soka.

Naye Kocha Mkuu wa Phantom FC, Mathias Wandiba alisema kiufundi timu yake ipo vizuri na aliamua kukutana na Alliance FC kwa sababu ni timu bora kimpira, hivyo alitaka kupima kikosi chake ili kubaini mapungufu na mafanikio kwa ajili ya kujipanga katika ligi daraja la tatu inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Recommended for you