Michezo

Timu ya Pamba yatamba kuchukua pointi zote kwenye uwanja wa nyumbani

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Timu ya Pamba SC ya jijini Mwanza imesema itatumia vyema uwanja wa  nyumbani  wa Nyamagana, na kuchukua point tatu muhimu dhidi ya JKT Oljoro, katika ligi daraja la kwanza inayoendelea kutimua vumbi nchini.

Timu hizo ambazo zipo kundi C katika ligi hiyo, zitachuana vikali jumapili Novemba 12, kwenye uwanja wa  Nyamagana huku Pamba SC wakiwa wenyeji wa  mchezo huo dhidi ya JKT Oljoro.

Hayo yalibainishwa na Afisa Habari wa Pamba SC, Johnson James wakati akizungumza na BMG.

James alisema kitu kinachowapa imani ni kutokana na mechi yao ya kwanza kukutana na timu hiyo, katika uwanja wa  Ushirika Moshi ambapo walitoka sare,hivyo watatumia uwanja wa nyumbani kushinda.

Alisema, watapambana kupata pointi tatu muhimu ili kufikisha jumla ya ponti 12 wakati ligi ikisimama kupisha usajili wa dirisha dogo, hali itakayosaidia kupunguza presha ya kushuka daraja.

Pia alisema, wanaendelea kujipanga ili wafanye vizuri na kuweza kusalia na wasishuke daraja japo zipo timu zaidi ya nne ambazo zinaweza kushuka,  na kwa sasa timu ipo vizuri kwani hawana majeruhi na kikosi kipo kambini kikiendelea na mazoezi chini ya Kocha  Venance Kazungu.

Hata hivyo alisema, baada ya kufanya vibaya mzunguko wa  kwanza mashabiki  wa  timu hiyo walijiweka pembeni,hivyo aliwaomba wajitokeze kwa wingi ili kuhamasisha timu na hatimaye kupata ushindi ambao ndio raha ya ushabiki.

Recommended for you