Habari Picha

Uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi mkoani Geita

on

Na Consolata Evarist, Geita

Jumuiya ya umoja wa wazazi wa chama cha mapinduzi(CCM) Mkoa wa Geita  imefanya  uchaguzi wa mwenyekiti na wajumbe wa mkutano Mkuu ambapo katika uchaguzi huo,Bw Lucas Singu Mazinzi aliibuka mshindi kwa kupigiwa kura 250.

Akitangaza matokeo katika uchaguzi wa kumchagua mwenyekiti mpya wa jumuiya hiyo    ,msimamizi wa uchaguzi   ambaye  ni Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu Donald Magesa  , alisema kura ambazo zilipigwa ni 320  na ambazo ziliharibika ni 19  kura harari 301.

Alisema kuwa   ,Lucas Singu   ameshinda dhidi ya wagombea wenzake   Hewa Samweli Masatu  aliyepata kura 36 na Mayengo Simion Kitindi ambaye alipata kura 15.

Aidha Magesa aliendelea  kutaja  nafasi za   wajumbe watakaowakilisha mkutano mkuu Taifa kutoka kwenye jumuiya hiyo, kuwa ni Ibrahimu Jumu Ibrahimu   Kura 38 , John Kafimbi Saulo kura 11, Charles Kazungu Mabeyo kura 192 na Rose Venasi Mweko  55.

Awali mbunge wa jimbo la Bukombe ambaye amemaliza nafasi yake ya uenyekiti wa jumuiya hiyo Doto Biteko,alisema   ndani ya kipindi chake cha uongozi amejidhatiti katika kuleta maendeleo ndani ya jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kuwa na miradi ambayo ni endelevu mfano uwanja ambao upo kwenye Wilaya ya Bukombe ambacho kinatarajia kujengwa chuo na kusimamia shughuli zote za maeneo ya uchimbaji madini ya dhahabu yanayomilikiwa na jumuiya hiyo.

Aliongeza kuwa anaamini ambaye amechaguliwa kurithi kiti chake hataweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kukamilisha pale ambapo ameishia.

Aidha Mwenyekiti wa  jumuiya hiyo ambaye amechaguliwa,Bw  Singu mbali na kuwashukuru wajumbe ambao wamempatia ushindi huo ,alisema mikakati aliyonayo ni kutafuta miradi mikubwa zaidi ndani ya jumuiya ikiwa ni pamoja na kukisaidia chama hicho kutimiza malengo yao.

Pia amewashukuru Wagombea wenzake ambao alikuwa akichuwana nao kwenye kinyanganyiro hicho kwa kukubaliana na matokeo ambayo yametangazwa.

Recommended for you