Michezo

Halmashauri ya Misungwi yaibuka bingwa mashindano ya UMITASHUMTA

on

Judith Ferdinand, BMG

Mashindano ya Umoja wa Michezo kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) 2018 ngazi ya mkoa wa Mwanza yamefika tamati kwa halmashauri ya Misungwi kuibuka mabingwa.

Kwenye kilele cha mashindano hayo juzi, Misungwi iliongoza katika michezo 13 na kujinyakulia vikombe  14 pamoja na kikombe kimoja cha ushindi wa jumla.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mabingwa hao, Afisa Michezo wa wilaya ya Misungwi Sixbert  Mbwambo alisema mashindano yalikuwa na ushindani mkali huku yakishirikisha wanafunzi bila mamuluki hivyo maandalizi mazuri ya halmashauri yake yamesaidia ushindi huo kupatikana.

Alisema wamejipanga kuwakilisha vyema mkoa katika mashindano hayo ngazi ya taifa kwani halmashauri hiyo imetoa washiriki 27 ambao wamefanya vizuri miongoni mwa 120 wanaounda timu ya mkoa wa Mwanza.

Mratibu wa mashindano hayo ngazi ya Mkoa, Joseph Mambo alisema mashindano hayo yalishirikisha michezo mbalimbali ikiwemo  mpira wa miguu, wavu, mikono, kengele, riadha kwa wavulana na wasichana, mpira wa miguu maalum kwa wavulana, pete,riadha maalum kwa wasichana na wavulana na sanaa za maonyesho huku jumla ya 1061 walishiriki huku wanamichezo 935 na viongozi 126.

Baadhi ya washiriki wa mashindano hayo kutoka Misungwi walieleza kufurahishwa na ushindi huo na kwamba wataendelea kuonyesha juhudi zaidi kupitia mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya taifa kwani hiyo ni fursa kubwa wao kuonyesha vipaji walivyonavyo.

SOMA Mashindano ya UMITASHUMITA ngazi ya wilaya Ilemela yaibua vipaji zaidi

Recommended for you