Habari Picha

Upanuzi wa barabara ya Makongoro hadi uwanja wa ndege wa Mwanza.

on

Judith Ferdinand, BMG

Utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa barabara ya Makongoro hadi uwanja wa ndege unatarajia kukamilika mwezi Mei mwaka huu.

Mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo ulisainiwa April 18 mwaka 2017 na unatekelezwa na kampuni ya Nyanza Road Work Ltd kwa zaidi ya shilingi bilioni tisa (Tsh. 9,542,701,531.96) ukisimamiwa na kitengo cha ushauri wa kihandisi cha wakala wa barabara TECU.

Akizungumza kwenye kikao cha pili cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mwanza kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Meneja wa TANROADS mkoa wa Mwanza Mhandisi Marwa Rubirya alisema hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 74 ambapo ujenzi wa barabara hiyo kuanzia Mwaloni-Furahisha na Pasiansi hadi uwanja wa ndege upo katika hatua nzuri.

Mhandisi Rubirya alisema uwekaji wa tabaka la lami ngumu umefikia urefu wa km 2.2, lami ya awali urefu wa km 2,9, tabaka la mawe yaliyosagwa urefu wa km 2.9, tabaka la msingi wa barabara km 3.1 na ujenzi wa daraja la Ilemela umekamilika kwa asilimia 90 hivyo utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 2 mwaka huu.

Hata hivyo alisema usanifu wa kina wa upanuzi wa daraja la Mabatini lililopo barabara ya Mwanza- Musoma utakamilika mwezi aprili mwaka huu na kazi inaendelea chini ya Mkandarasi Mshauri kampuni ya Advance Engineering Solution kwa zaidi ya shilingi Milioni 200 (Tsh.Milioni 242,574) hii ni kutokana na kuwepo tatizo la mafuriko kwa muda mrefu kwenye daraja hilo pindi mvua zinaponyesha na kusababisha maji kupita juu ya barabara kwa kuwa na upana mdogo ya kupitishia maji.

Aidha alisema matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa kazi zao ni kuchelewa kutolewa kwa fedha za matengenezo ya barabara na usimamizi na zinazotengwa ni kidogo ukilinganisha na mahitaji halisi pamoja na mchakato wa manunuzi kutumia muda mrefu hivyo kupunguza muda wa utekelezaji.

Vilevile alisema ofisi ya meneja mkoa kwa kushirikiana na wahandisi washauri wataendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yote ili ikamilike kwa wakati kama ilivyopangwa hivyo kwa kuiwezesha ofisi yao kutekeleza majukumu  ya kujenga na kusimamia matengenezo ya barabara kama ilivyoidhinishwa katika bajeti ya wizara yao wanashauri fedha zitolewe kwa wakati.

Kwa upande wake Mratibu wa  Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mwanza, Francisco Magoti alisema dhima yao ni kupanga, usanifu, ujenzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara za Vijijini  na Mijini kwa kuzingatia ufanisi wa gharama kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi nchini.

Alisema TARURA ina mtandao wa barabara wenye urefu wa km 4891.56 kwa halmashauri zote za mkoa huo ambapo barabara ya lami km120.41, barabara ya mawe km 8.537, barabara ya zege km 2.51, barabara za changarawe km 1525,673 na barabara ya udongo km 3235,22.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, John Wanga aliomba kipande kitakacho baki cha barabara ya Buswelu hadi Igoma nacho kijengwe kwa kiwango cha lami ili kuleta taswira nzuri na wananchi kufanya shughuli za uchumi kwa urahisi baada ya kukamilika kwa mradi wa barabara ya Buswelu kupitia Kiseke mpaka Sabasaba ambao unatarajia kuanza mwezi Mei, huku Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mary Tesha aliwaomba TARURA kuendelea kushirikiana na  wakuu wa wilaya na wabunge katika kutekeleza majukumu yao.

Recommended for you