Michezo

Usajili Rock City Marathon 2018 waanza rasmi

on

Na Mwandishi Maalum

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mheshimiwa John Mongella amekuwa mshiriki wa kwanza kujisajili kushiriki mbio za Rock City Marathon zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu katika viwanja vya CCM Kirumba.

Akizungumza kwa niaba ya RC Mongella kwenye hafla fupi iliyofanyika Setemba Mosi, 2018, Mkuu wa Wilaya Nyamagana Mhe. Dkt. Philis Nyimbi alitoa wito kwa wadau wa michezo na utalii katika Kanda ya Ziwa kuhakikisha wanayatumia vizuri mashindano hayo katika kutangaza fursa na vivutio vya utalii na kukuza mchezo wa riadha.

Pia aliwapongeza waandaaji wa mbio hizo kampuni ya Capital Plus International na kutoa rai kwa waandaaji  hao kushirikiana na viongozi wa mchezo wa riadha nchini kuhakikisha wanakuwa na mkakati wa kudumu unaolenga kuwaandaa washiriki kutoka ndani ya nchi ili waweze kuleta matokeo mazuri dhidi ya washiriki kutoka mataifa ya nje.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mbio hizo, Zenno Ngowi aliwasihi washiriki wanaotoka ndani ya nchi kufanya maandalizi ya kutosha kutokana na ushindani mkubwa unaotarajiwa kutoka kwa washiriki wa nje ya nchi ambao, kwa mujibu wake wameonesha mwitikio mkubwa wa kushiriki katika mbio hizo.

Alivitaja vituo vitakavyohusishwa katika usajili huo kuwa ni pamoja na Igoma, Buzuruga, Airport Mwanza, Rock city mall, Chuo Kikuu cha Saut, Nyegezi Stand, Mwanza hotel, Nyamagana Stadium, Dampo pamoja na Nyakato. Alisema usajili huo pia utahusisha ofisi zote za riadha mikoa ya Geita, Simiyu na Shinyanga.

Alisema usajili huo utahusisha mbio za km 42 kwa wanaume na wanawake, Kilomita 21 kwa wanaume na wanawake, km 5 kwa washiriki kutoka kwenye mashirika (Corporates) na walemavu wa ngozi, km 3 kwa wazee wenye umri kuanzia miaka 55 na kuendelea pamoja na km 2.5 kwa watoto wenye umri wa miaka 7 hadi 10.

Recommended for you