Habari Picha

Vijana wa UVCCM wilayani Magu wazidi kuimarika kiuchumi

on

Judith Ferdinand, BMG

Chama cha Mapinduzi CCM katika wilaya ya Magu mkoani Mwanza kimekabidhi mashine ya kuchomelea (Welding Machine) kwa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCC) Kata ya Kahangara ili kuwasaidia kujiimarisha kiuchumi.

Mashine hiyo ilikabidhiwa juzi kwenye uzinduzi wa kambi UVCCM Kata ya Kahangara ambapo Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Magu, Ayoub Bindulle alisema lengo la kambi hiyo ni kuwaandaa vijana kujua itikadi na namna chama kilivyo, kusimamia sera, ilani pamoja na kulinda chama na serikali.

Bindulle alisema katika kambi hiyo pia vijana wamepata  mafunzo ya kijamii, kimwili, kiakili, ujasiriamali, kujitunza na kuitaka kamati ya utekelezaji ya Kata hiyo kuunda kamati ya uchumi itakayoshugulikia masuala ya uchumi.

Katibu wa CCM wilaya ya Magu Edward Mamba alisema wamejipanga kisiasa na kiuchumi hivyo watasimamia vyema mashine waliyokabidhiwa na kwamba itakuwa chanzo kikuu cha mapato ya vijana wa Kata ya Kahangara.

Mmoja wa washiriki wa kambi hiyo Pendo Mashiku alieleza kupata mafunzo na elimu ya kijinsia, ujasiriamali na amejifunza aina za ukatili na namna ya kujilinda hivyo ataitumia elimu hiyi kuwaelimisha wenzake.

Mwenyekiti wa kambi hiyo Edward James alisema mashine waliyopewa wataifanyia kazi kama ilivyokusudiwa na wataonyesha mfano bora katika jamii ili kuonyesha CCM inawajali vijana na inataka wafanye kazi kwa bidii.

Naye Katibu Mwenezi wa CCM wa Kata ya Kahangara, Joseph Manyama alisema mafunzi hayo ni ya siku saba na yameshirikisha vijana 105 kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita na waliomaliza shule huku akiomba serikali kuwapa kipaumbele inapotokea fursa ya mafunzo ya JKT kwani wanayahitaji.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi CCM wilayani Magu, Bubele Bubele alitoa rai kwa vijana walio shule kuzingatia masomo na walio nje ya shule waendelee kujiendeleza huku wakifanya kazi kwa bidii kama ilivyo ilani ya CCM.

Mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kambi ya UVCCM Kata ya Kahangara alikuwa Abel Mahenge ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa na pia Katibu wa Elimu na Uchumi wilaya ya Kwimba ambapo alisema mashine waliyokabidhiwa vijana hao ina thamani ya shilingi 350,000 lengo likiwa ni kuwahamasisha vijana ili waweze kujiajiri na kujitegemea kiuchumi.

Recommended for you