Michezo

Timu ya soka ya SAUT FC yadoda michuano ya Rock City Cup 2018

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Timu ya Bifad FC imeilaza timu ya SAUT FC kwa kichapo cha goli 3-2 katika mchezo wa mashindano ya Rock City Cup 2018 yanayoendelea kutimua vumbi katika uwanja wa kisasa wa Nyamagana Jijini Mwanza.

Mchezo huo umezikutanisha timu kutoka kundi B huku kila moja ikiwa imecheza mechi mbili ambapo Bifad FC walifunga magoli kupitia washambuliaji wake Henry Gama, Naser Muzamir na Hajji Juma na SAUT FC wakipata magoli kupitia Philimon Lwambano na Felix Stephano.

Kocha wa Bifad FC Hassan Shekhata anasema mchezo ulikuwa mgumu ila walitumia madhaifu ya mabeki wa wapinzani wao na kushinda katika mchezo huo, hivyo wataenda hivyo hivyo hadi fainali na hatimaye kuibuka na ubingwa.

Kocha wa SAUT FC Joseph Budamu anasema walipoteza mchezo huo baada ya wapinzani wao kutumia madhaifu yaliyojitokeza hivyo atayafanyia kazi makosa hayo na kwamba mashabiki wasikate tamaa waendelee kuiunga mkono timu hiyo.

Ikumbukwe kuwa lengo la mashindano hayo ni kurudisha hamasa kwa wananchi kwenda viwanjani kuangalia mechi kupitia kampeni ya “Uzalendo kwanza, Twende zetu viwanjani”, kuendeleza vipaji vya soka.

Recommended for you