Audio & Video

Wasaidizi wa kisheria wilayani Magu wataka elimu zaidi

on

Wasaidizi wa kisheria ngazi ya jamii kutoka Kata za Bujashi na Lutale wilayani Magu wakijengewa uwezo wa kisheria na shirika la Haki Zetu kupitia mradi wa “Vitendo Vidogo Vidogo Vinaleta Mabadiliko (Actions Brings Changes)”.

Judith Ferdinand, BMG

Wasaidizi wa kisheria ngazi ya jamii (Paralegals) kutoka Kata za Bujashi na Lutale wilayani Magu wametoa rai kwa shirika la Haki Zetu kuongeza muda wa kuendelea kutoa mafunzo kuhusiana na masuala ya sheria.

Wasaidizi hao walikuwa wakipatiwa mafunzo na shirika hilo kupitia mradi wa “Vitendo Vidogo Vidogo Vinaleta Mabadiliko (Actions Brings Changes)”, ambao uliweza kuwajengea uwezo wasaidizi wa kisheria ngazi ya jamii 30 na viongozi mbalimbali ikiwemo wenyeviti wa vijiji ili kusaidia jamii kuhusu masuala ya kisheria

Akizungumza juzi wakati wa kikao cha tathimini juu ya mradi huo ulioanza Machi hadi Mei mwaka huu, Dotto Sengerema ambaye ni msaidizi wa kisheria alisema bado wanalihitaji shirika hilo hivyo aliomba liongeze muda wa kuendelea kuwafundisha zaidi kuhusiana na sheria ili wapate mwanga utakaosaidia jamii kuelewa na kupunguza vitendo vya unyanyasaji na uminywaji wa haki.

Sengerema alisema mradi huo umeleta mabadiliko makubwa katika jamii kwani wamepata elimu sahihi kuhusu utetezi wa kisheria ambapo wameweza kuwa wajasiri na kuripoti vitendo mbalimbali ikiwemo vya unyanyasaji wa kijinsia.

“Nalishukuru shirika la Haki Zetu kutuletea mradi huu ambapo elimu tuliyoipata nasi tukaipeleka kwa wanajamii wengine kupitia vikao mbalimbali”. Alisema Sengerema.

Naye Salma Juma alisema kabla ya mradi huo hawakujua ni wapi waende endapo kunakuwa na vitendo vya unyanyasaji katika jamii ila sasa wamepata mwanga kwani wamefundishwa sheria ndogo ndogo  na namna ya kupata msaada wa kisheria hasa vijijini.

Juma alisema tangu wajengewe uwezo kama wasaidizi wa kisheria ngazi ya jamii wameweza kusuluhisha na kutatua migogoro ya ardhi, ukatili wa kijinsia kwa wanawake, watoto na wazee, na kwamba jamii imepata uelewa wa kujua muelekeo wa kesi zao, wapi pa kuanzia na nani wa kumuoana endapo wanahitaji msaada wa kisheria.

Mmoja wa wananchi kutoka Kijiji cha Kayenze B Kata ya Lutale, Joseph Mabula alisema jamii imenufaika  kwa kuondolewa uoga wa kuripoti matukio ya uvunjifu wa sheria na kupata ufahamu kuwa watoto hawana haki ya kugombania mali za wazazi kama wapo hai kwani jambo hilo lilikuwa tatizo hapo awali.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Lutale, Devotha Robert aliliomba shirika hilo kuwatafutia wasaidizi hao wa kisheria ofisi ili waweze kutambulika kwa jamii na  kuwafikia watu wengi kwani wananchi  watakapokuwa na shida wataenda moja kwa moja tofauti na wao kuwafuata majumbani mwao.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Kijiji cha Sese kilichopo Kata ya Bujashi, Simon Anacret alisema  tangu kuanza kwa mradi huo jamii imeanza kupata mwamko kwa kuripoti vitendo vya ukatili, pia wasaidizi wa kisheria wamekuwa wakiwasaidia kupunguza kazi kwani wamekuwa wakipokea kesi mbalimbali ikiwemo za migogoro ya ardhi na kuziwasilisha kwao.

Meneja Miradi shirika la Haki Zetu, Gervas Evodius alisema mwitikio umekua mkubwa na uelewa umeongezeka kwa wananchi kuripoti vitendo vya ukatili ambapo mpaka mradi unakamilika kwa awamu ya kwanza wameweza kupokea kesi 46 ambazo wamesuruhisha na kumalizika huku nyingine zikiwa katika hatua mbalimbali.

Evodius alisema mradi utaendelea baada ya tathimini ili kujua walipofanikiwa kwa awamu ya kwanza na mapungufu yaliyojitokeza ili wakati ujao waboreshe zaidi na kuwafikia wananchi wengi.

ISOME PIA HABARI HII Mwanza kuadhimisha Siku ya Hedhi Duniani 2018 

Recommended for you