Habari Picha

WACHUNGAJI WA MAKANISA YA EAGT WATAKIWA KUTOITAMBUA KATIBA MPYA.

on

Askofu Mkuu Msaidizi wa dhehebu la EAGT nchini,John Mahene (pichani), amewataka wachungaji wa makanisa ya dhehebu hilo kutoitambua katiba mpya ya EAGT iliyopitishwa hivi karibuni mjini Dodoma.

Askofu Mahene ameyasema hayo hii leo Jijini Mwanza wakati akizungumza na wanahabari katika kanisa la EAGT Bugando.
Amesema katiba hiyo inayozuia viongozi wa dhehebu hilo kuwa na umri usiozidi miaka 70 imelenga kukwamisha utendaji kazi wake baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Mwanza kusimamisha maamuzi ya kutenguliwa kwake kutokana na kashfa za kiuongozi zinazomkabiri hadi kesi iliyo mahakamani itakapotolewa maamuzi.

Amebainisha kwamba hayo yanafanyika ili kumkwamisha kujua yanayotendeka ndani ya uongozi wa EAGT ikiwemo ununuzi wa magari takribani 50 tangu mwaka 2005 hadi 2016 ambayo hata hivyo hajawahi kuyaona.

Itakumbukwa kwamba Septemba 17,2016 Askofu Mahene alisimamishwa uongozi katika maamuzi yaliyofikiwa na baadhi ya viongozi wa dhehebu la EAGT ambao ni Askofu Mkuu, Katibu Mkuu, Mtunza Hazina na Mshauri wa Kanisa kutokana na tuhuma za mmoja wa watumishi ya makanisa ya EAGT kwamba ameota ndoto kuwa kiongozi huyo amezaa nje ya ndoa yake jambo ambalo ni kinyume na maadili ya uongozi wa dhehebu hilo.

Hata hivyo alifungua kesi ya udharirishaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Mwanza ambayo ilizuia kusimamishwa uongozi wake hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuru aendelee kupata stahiki zote kama Askofu Mkuu Msaidizi wa EAGT nchini.

Licha ya hayo, Februari 22 mwaka huu baadhi ya wachungaji na viongozi wa EAGT walikutana Mjini Dodoma katika mkutano wa mabadiliko ya katiba mpya ya dhehebu hilo bila kumshirikisha Askofu Mahene ambaye bado anaendelea kupigania uhalali wa uongozi wake ikiwemo kufungua kesi ya ukiukwaji wa katiba katika Mahakama Kuu Jijini Dar es salaam.

Askofu Mkuu Msaidizi wa dhehebu la EAGT, Baba Askofu John Mahene (katikati), akizungumza na wanahabari Jijini Mwanza. Kushoto ni Shemasi Daudi Kolyi na kulia ni Mzee wa Kanisa Paul Mtoka.
Askofu Mkuu Msaidizi wa dhehebu la EAGT, Baba Askofu John Mahene (katikati), akizungumza na wanahabari Jijini Mwanza.
Askofu Mkuu Msaidizi wa dhehebu la EAGT, Baba Askofu John Mahene, amesema alisimamishwa kinyume cha katiba na Askofu Mkuu, Katibu Mkuu, Mtunza Hazina na Mshauri wa Kanisa. Amesema ilipaswa maamuzi hayo yafanywe kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu na baadaye Mkutano Mkuu.
Binagi Media Group

Recommended for you