Habari Picha

WADAU WA ELIMU MKOANI MWANZA WATAKIWA KUWA WABUNIFU

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Walimu, wanafunzi na wadau wa elimu mkoani Mwanza wametakiwa kutumia fikra zao kubuni mawazo yatakayosaidia kuelekea Tanzania ya viwanda na uchumi  wa kati, itakayokuwa na uwezo wa kujitegemea bila wahisani na hatimaye kusaidia kutatua tatizo la ajira nchini.

Wito huo ulitolewa jana na   Mratibu wa maonyesho ya elimu yanayofanyika mkoani Mwanza ambaye ni  Mkurugenzi wa Kuboja Entertainment,  Kulwa Kuboja yaliyoanza Oktoba mosi hadi tano yanayofanyika katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.

“Ili kufikia uchumi wa viwanda na kati,inatakiwa walimu,wanafunzi na wadau wa elimu kubuni mawazo ambayo yatasaidia kufikia malengo,sambamba na vijana kutumia elimu zao kuboresha biashara wanazofanya wazazi wao na wajasiriamali,” alisema Kuboja.

Kuboja alisema, maonyesho hayo yamelenga kutoa fursa kwa walimu,wadau na ofisi ya  elimu,wazazi,walezi na wanafunzi kukutana na kukaa pamoja,kubadilishana mbinu na uzoefu katika malezi,ufundishaji na kujifunza ili kuleta matokeo bora ya elimu katika mkoa wa Mwanza na taifa kwa ujumla sambamba na  kubuni mawazo yatakayosaidia kufikia uchumi wa viwanda na kati.

Alisema, maonyesho hayo yanaenda sambamba na uuzaji wa  zana za kufundishia na kujifunzia zipatikanazo madukani.

Pia alisema, kutakua na mashindano ya zana za kufundishia na kujifunzia zitakazobuniwa na wanafunzi kwa msaada wa walimu shuleni,vyuoni pamoja na vikundi mbalimbali vya sanaa na wabunifu toka shule zilizopo mkoani Mwanza.

Hata hivyo alisema, kupitia maonyesho hayo yatatoa fursa kwa walimu kuonyesha uwezo wao katika kutumia zana za kufundishia kulingana na maendeleo ya sayansi na teknolojia,kuendana na mtaala wa elimu nchini, na taasisi binafsi za elimu kukutana na kubadilishana mikakati ya uboreshaji elimu na mahusiano baina yao na wananchi.

Aidha alisema,  yatatumika kuibua vipaji vya wanafunzi katika nyanja mbalimbali,ambapo kila shule imeelekezwa kuwabainisha na kuwaandaa wenye vipaji maalumu kama vile matumizi ya lugha,uchoraji,ubunifu wa kiteknolojia,uandishi wa habari, uandishi wa insha,tenzi,tungo,hadithi,mashairi pamoja na nyimbo,ili kutambulisha vipaji vyao na kuviendeleza.

Recommended for you