Michezo

Wadau wa Michezo Mwanza wapewa NENO

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Wadau wa  michezo nchini wameombwa kusapoti na kujitokeza kudhamini mashindano mbalimbali ya kuibua vipaji katika mkoa wa Mwanza.

Hii itasaidia kukuza na kuendeleza vipaji katika mkoa wa Mwanza na siyo kuishia kuunga mkono mkoa wa Dar es salaam.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya timu ya  Kona FC na  Mwanza City  katika mashindano ya chini ya umri wa  miaka 12 na 15 yanayoendelea kutimua vumbi kwenye uwanja wa Nyamagana Kocha  wa  Kona FC ya chini  ya miaka 15  Hamis Omary alisema, wadau wajitokeze kusapoti mashindano hayo na mengine kwa ajili ya kuibua vipaji na kuviendeleza mkoani hapa.

Omary alisema, Mwanza kuna vipaji ila tatizo hakuna wadhamini wanaowashika mkono na badala yake wanaishia Dar es salaam tu.

Hata hivyo alisema, ni wakati wa wadau hao kuona umuhimu wa kusapoti mkoa wa  Mwanza kimichezo, ili uweze kuwakilisha vyema katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Pia alisema, kupitia  mashindano hayo ya ligi kwa watoto waliochini ya umri wa miaka 12 na 15, yatasaidia watoto hao kuonyesha vipaji walivyonavyo katika soka, sambamba na kuomba waandaaji wasiishie hapo bali waandae na mengine kwa vijana wenye umri zaidi ya 15 ili kupata timu bora katika makundi mbalimbali watakao weza kushiriki mashindano na ligi tofauti ndani na nje ya nchi.

Recommended for you