Habari Picha

Wafanyakazi wa Shirika la WOTESAWA wadhimisha “Jumanne ya Utoaji”

on

Leo Novemba 28,2017 ilikuwa “Jumanne ya Utoaji/Kulitolea” (Giving Tuesday) 2017, ambapo wafanyakazi wa shirika la Kutetea Haki za Watoto Wafanyakazi wa Nyumbani WOTESAWA, wametembelea watoto/wanafunzi wenye ulemavu katika shule ya St.Magdalena Wa Canose Igoma Jijini Mwanza na kutoa zawadi na mahitaji mbalimbali.

Siku hii huadhimishwa duniani kila jumanne ya mwisho wa mwezi Novemba, ambapo wanajamii/taasisi na wadau kadha wa kadha husaidia mahitaji mbalimbali kwa watu wenye uhitaji.

Mkurugenzi wa shirika la WOTESAWA, Angel Benedicto amewapongeza waalimu wa shule hiyo kwa namna wanavyowalea vyema watoto hao na kuhimiza kwamba kupitia siku hii ni vyema wanajamii wakawa na desturi ya kuwasaidia wahitaji.

Naye Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka shirika la WOTESAWA, Elisha David amebainisha kwamba miongoni mwa mahitaji yaliyokabidhiwa shuleni hapo ni pamoja na chupa 20 za mafuta ya Oliva, mabegi 20 ya watoto, madaftari katoni moja na zawadi mbalimbali ikiwemo juisi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa shule hiyo, Mlezi wa darasa la awali la watoto walevu na wenye mtindio wa akili, Mwl.Agatha Chandulu ameshukuru kupokea mahitaji hayo kutoka WOTESAWA na kuwahimiza wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu kutowaficha nyumbani na kuwakosesha haki ya kupata elimu.

Katika ugeni huo, kila mmoja amevutiwa na vipaji walivyonavyo watoto hao ikiwemo uimbaji wa mtoto Getruda Laurance (06) ambaye amepoteza uwezo wa kuona lakini amejaaliwa kipaji cha uimbaji pamoja na kuwatambua kwa majina wanafunzi na waalimu wake kwa kuwagusa.

Recommended for you