Audio & Video

Wahanga wa Fidia Geita wapata matumaini mapya

on

Na Joel Maduka, Geita

Naibu  waziri wa madini  Stanslaus Nyongo amesema kuwa serikali ya awamu ya tano haiko tayari  kuona mtu akilalamika ,kunyanyaswa au kunyimwa haki yake.

Kauli hiyo aliitoa wakati akiongea na wananchi wa Kijiji cha Nyakabale, Kata ya Mgusu wilayani Geita wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani hapa, kuzungukia maeneo ya wachimbaji pamoja na kusikiliza kero za wananchi ambao wanazunguka kwenye baadhi ya maeneo ya mgodi wa Geita (GGM).

Hatua  hiyo ya Naibu waziri Nyongo imekuja baada ya kusikia malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya mgodi wa GGM kushindwa kuwalipa fidia kwa muda mrefu pamoja na kuwepo kwa maagizo mengi ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakifika Mkoani Humo.

Naibu waziri alisema kuwa mtu mwingine yuko tayari kuona mtanzania mwenzake akikandamizwa ili yeye  aendelee kulinda masilahi yake  binafsi na kwamba miaka hiyo imeshapita muda uliopo kwa sasa ni kufanya kazi za kuwatumikia wananchi ambao ni wanyonge.

“Tukikaa kwenye viyoyozi hatuambiwi ukweli na wamiliki wa migodi lakini tunapo fika katika eneo husika tunapata ukweli, unakuta mtu kazaliwa hapo kakulia hapo amejenga ana watoto harafu mtu anakuondoa kwa madai kuwa upo kwenye leseni yake  ainiingi akilini kama unahitaji eneo langu njoo tukae tumalizane  unipe changu mimi nisepe inakuwa nilipe nisepe ”alisema Nyongo.

Hata hivyo aliwataka watu wa mgodi huo kuwalipa wananchi hao ama waondoke wawaachie wananchi hao eneo lao waendelee kuchimba na sio kuwazuia ikiwa hawafanyi shughuli za uchimbaji kwa sasa au wawaache waendelee kufanya shughuli za bila kubuguziwa,  mgodi ulikuja kama neema hivyo isiwe mgodi huu kazi yake  kuwanyanyasa wananchi.

Awali akitoa malalamiko kwa Naibu Waziri, mmoja wa mwananchi wa Nyakabale, Joseph Kihengu aliitupia lawama serikali iliyopita akisema inawezekana wakati wanabinafsishamgodi wa GGM na wao walibinafisishwa humo bila kujua.

“Mheshimiwa kipindi cha nyuma usingeweza kupata umati kama huu, umati huu umetokana na imani ya serikali ya awamu ya tano waliyo nayo hivyo serikali iwaangalie kwa jicho la tatu ili watu wanyakabele wajue hatima ya maeneo ambayo yapo ndani ya bikoni za mgodi wa GGM”. Alisema Kihengu.

Katika hatua nyingine akina mama wa Nyakabale wakiwakilishwa na Godliva Mgini waliutupia lawama mgodi huo wa GGM kwa kukilaghai kikundi chao cha Baraka baada ya  kuahidiwa kuwezeshwa ili kuanzisha mradi wa ufungaji wa nguruwe 100 ambapo waliambiwa wasombe mawe ili wajenge na kujikuta wakighalamia kiasi cha shilingi laki nane  baadae wakatokomea kusiko julikana na kuwaacha maskini zaidi.

Nae Makamu wa Rais Mgodi wa GGM, Saimon Shayo alisema “baadhi ya maneno yaliyoelezwa hapa mengine yanafahamika mengine ni mageni ndo tunayasikia na mengine tunahitaji kama mgodi kukaa na kuyapatia ufumbuzi”.

Recommended for you