Habari Picha

WAJASIRIAMALI WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA KUTOKA TBS

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Ili kuchochea Maendeleo ya viwanda nchini, wafanyabiashara na wajasiriamali wameshauriwa kuthibitisha ubora wa bidhaa zao kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Ushauri huo ulitolewa jana na Kaimu Mkuu TBS Kanda ya Ziwa, Joseph Makene wakati akizungumza na BMG katika Maonyesho ya 12 ya Afrika Mashariki yanayofanyika kwenye uwanja wa Rocky City Mall Jijini Mwanza, yalioandaliwa na Tanzania Chamber of Commerce, Industry and Agriculture (TCCIA) ambapo yalianza Agosti 25 mpaka semptemba 03 mwaka huu.

Makene alisema TBS  ina utaratibu wa kukagua na kuthibitisha ubora wa bidhaa kutoka kwa wazalishaji wadogo, wa kati na wakubwa ili kupatiwa leseni inayomruhusu kutumia nembo ya ubora na kumsaidia kuuza bidhaa zake ndani ya nchi pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema wafanyabiashara na wajasiriamali wanaweza kuuza bidhaa zilizothibishwa na kuwa na nembo ya TBS kokote ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jambo litakalosaidia kuendeleza viwanda kwani  kupitia jumuiya hiyo bidhaa itakayo thibitishwa na shirika la viwango la nchi husika itauzwa popote.

Alidokeza kwamba hiyo ni fursa ambayo wajasiriamali wanatakiwa kuitumia ili kukuza na kupanua wigo wa soko la ndani ya nchini na nje ya nchini ikiwemo kwenye nchi za Afrika Mashariki ambapo kuna soko kubwa kwa ajili ya kuuza bidhaa zao.

Aidha alisema kwa wajasiriamali wadogo ambao wanatambuliwa na SIDO wanathibitishiwa bila malipo na hivyo kuwataka kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kupata leseni ya ubora ili kusaidia kuuza bidhaa zao katika soko la Jumuiya hiyo sambamba na kuleta maendeleo ya viwanda nchini.

“TBS inapenda kuwakumbusha wajasiriamali wadogo kuwa serikali kupitia TBS hutenga pesa kwa ajili ya kugharamia uthibishwaji ubora wa bidhaa zao, kigezo ni kuwa na leseni ya biashara, barua ya utambulisho kutoka SIDO kuwa wewe ni mjasiriamali na cheti cha TFDA kwa wazalishaji wa bidhaa za chakula, hivyo ni wakati wa kutumia fursa hiyo kwa maendeleo ya viwanda na soko ya Afrika Mashariki,” alisema Makene.

Hata hivyo alisema TBS inaunga mkono kipaumbele cha Rais John Magufuli cha maendeleo ya viwanda kwani uthibitishaji ubora wa bidhaa kunachangia kuleta maendeleo hayo maana bidhaa hizo zinakubalika katika soko la jumuiya hiyo.

Vilevile alisema dhima ya shirika hilo ni kukuza matumizi ya viwango na kanuni za udhibiti ubora katika sekta ya viwanda na biashara kupitia ukuzaji wa matumizi ya viwango, utoaji wa leseni kwa bidhaa zinazokidhi ubora, ukaguzi upimaji na ugezi ili kuchochea maendeleo endelevu ya taifa kiuchumi.

Recommended for you