Makala

Mradi wa nyumba za makazi Magomeni Kota waleta matumani makubwa

on

Mtendaji Mkuu Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch.Elius Asangalwisye Mwakalinga aonyesha uwezo mkubwa katika kusimamia ubora wa miradi na kuokoa fedha za umma.

Na Mwandishi Maalum

Nimepitia taarifa ya maendeleo ya mradi mkubwa wa nyumba za makazi ujulikanao kama “Mradi wa Nyumba za Makazi Magomeni Kota”. Kilichonifurahisha ni namna ambavyo Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch.Elius Asangalwisye Mwakalinga alivyochukua hatua mbalimbali katika kuokoa fedha za Umma na kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora licha changamoto mbalimba wanazokutana nazo wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Katika taarifa hiyo fupi ya utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa kwa pamoja na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara ya Fedha na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambapo kila mmoja akiwa na majukumu yake maalumu  kwenye mradi huo.

Utekelezaji wa mradi huo ulianza kwa wataalamu wa TBA kufanya ubunifu wa majengo na wale wa BICO-UDSM kufanya uchunguzi wa udongo ili kubaini uwezo (Bearing Capacity) wa kuhimili uzito wa majengo unaotarajiwa kujengwa, wakati huo huo wakala wa majengo aliendelea kufuatilia vibali kutoka mamlaka mbalimbali zikiwemo NEMC, Manispaa, AQRB na ERB haya yote yalifanyika ili kukidhi mahitaji ya kisheria kwenye sekta ya ujenzi.

Mradi huu una jumla ya vitalu  vitano (5 Blocks) ambapo vitalu vinne vina ghorofa nane na moja ina ghorofa tisa ambapo kitaru kimoja kinabeba  Kaya 126 na kufanya kuwa mradi mkubwa na wa kisasa kwa hapa nchini. Mradi mzima unauwezo wa kubeba Kaya 656 maana vitalu vinne vinabeba Kaya 512 na kitalu kimoja kina uwezo wa kubeba Kaya 144.

Hadi sasa mradi umeweza kukamilisha ujenzi wa msingi kwa asilimia mia moja (100%) na asilimia 35% kwa kazi ya juu ya msingi, kama kawaida yake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania  Arch.Mwakalinga amekuwa akifanya majaribio ya uchunguzi wa zana mbalimbali kwenye maabara mbalimbali ili kuhakikisha vifaa vya ujenzi kwenye mradi huo ni vyenye ubora unaohitajika kwa mujibu wa maelekezo ya kitaalamu, vifaa vinavyochunguzwa mara kwa mara ni kama vile mchanga, kokoto, nondo na zege ambapo maabara zilizotumika ni kama vile  Chuo kikuu cha Dar es Salaam, BICO, na DIT.

Tathimini ya gharama za mradi huo kulingana na tathimini iliyofanywa na wakadiriaji majengo ni kiasi cha shilingi za kitanzania 14,497,144,106.65. Mradi una jumla ya  “block” tano zenye jumla ya “floor” 41 mpaka sasa kati ya hizo “floor” 12 zimekamilika. Makisio ya gharama kwa “floor”  moja ni shilingi  438,611,875,00 hivyo basi  makisio ya gharama ili kuweza kumaliza  “floor” 29 zilizobaki ni shilingi 12,719,744,375.00 (shilingi bilioni kumi na mbili milioni mia saba kumi na tisa laki saba arobaini na nne mia tatu sabini na tano)

Hapa ndipo ninapo mpongeza Arch. Elius Asangalwisye Mwakalinga

Mtambo wa kisasa wa kuzalisha zege umeweza kuzalisha kiasi cha mita za ujazo 5,799.800 kwa miradi mbalimbali ya mkoa wa Dar es salaam kama vile Magomeni Kota, Ukonga, TPA, Bandari, Osha na Ujenzi wa nyumba ya Rais Mstaafu Mhe.Jakaya Mrisho Kikwete unaofanyika Kawe

Maamuzi ya kununua mtambo wa kuzalisha zege yaliyofanywa na Wakala wa Majengo Tanzania umeleta faida nyingi sana na kuokoa fedha nyingi ambapo moja ya faida hizo ni;

(a) Kupungua kwa gharama za uzalishaji  wa zege

(b) Kuokoa muda wa utendaji kazi

(c)Ubora wa zege kwa kuwa TBA wanazalisha wenyewe

(d) Matumizi sahihi ya malighafi kama kokoto, mchanga,na simenti.

Changamoto na utatuzi wake

Arch.Mwakalinga akiwaongoza wataalamu wenzake katika mradi huu alikumbana na changamoto mbalimbali  ikiwemo kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi, mfano bei ya awali ya nondo ilikuwa shilingi milioni moja laki sita na ishirini  mpaka milioni moja na laki nane na bei ya sasa ni shilingi milioni mbili laki mbili na elfu hamsini kwa tani.

Lakini kwa weledi mkubwa Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch.Mwakalinga aliweza kutatua changamoto hii kwa kupata wazabuni ambao wanasambaza vifaa kwa bei nafuu na maamuzi yenye busara kwa kununua mtambo na magari na kupunguza gharama za mradi.

Kuokoa fedha za umma

Kwa kutumia Wakala wa Majengo Tanzania chini wa uongozi wa kizalendo wa Arch.Mwakalinga, Serikali imeweza kuokoa mabilioni ya fedha kupitia miradi kadhaa ikiwemo;

  1. Ujezi wa Mabweni ya Chuo Kikuu ambapo Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) amejenga kwa shilingi bilioni 10 badala ya bilioni 80 za wakandarasi binafsi.

2.Ujenzi wa Shule ya Sekondari Ihungo, TBA wamejenga kwa shilingi bilioni 13 badala ya bilioni 40 za wakandarasi binafsi.

3.Ujenzi wa Hospitali mkoani Geita, Wakala wa Majengo Tanzania waliweza kujenga na kukamilisha kwa shilingi bilioni 17 badala ya shilingi bilioni 75 za wakandarasi binafsi.

  1. Ujenzi wa Hospitali wilayani Chato, Wakala wa Majengo Tanzania walijenga kwa shilingi bilioni 15 badala ya shilingi bilioni 65 za wakandarasi binafsi.
  2. Ujenzi wa Hospital mkoani Simiyu, Wakala wa Majengo Tanzania walijenga na kukamilisha kwa mradi kwa shilingi bilioni 12 badala ya shilingi bilioni 36 za wakandarasi binafsi

Ukipiga hesabu utaona TBA imeokoa kiasi kikubwa cha fedha za serikali ambazo zimeingia kuwahudumia wananchi kwenye miradi ya maendeleo. Kwa namna hii, kwa nini nisipoteze muda wangu kumpongeza mzalendo wa aina hii ya Arch.Mwakalinga?.

Jambo kama hili haliwezei kuwafurahisha wapigaji waliokuwa wakitaka Wakala wa Majengo Tanzania TBA aendelee kukodi mitambo na magari ili kuongeza gharama za mradi na wapo hata waheshimiwa wabunge wanatumika kufanya hujuma hizi. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo amemuunga mkono Rais Magufuli kwa kununua mtambo na siyo kukodi kwa sababu hata Mhe.Rais alipinga wazo la wabunge kukodi ndege na badala yake aliamua kununua kabisa ili kukwepa gharama na kutuleteaa maendeleo ya uhakika.

Katika kuiunga mkono TBA kwenye maendeleo ya mradi wa Magomeni Kota, Mbunifu Majengo anayeheshimika sana kwa uwezo wa kiutendaji Arch.Humphrey Zachary Killo amesema ”Mradi huu ni muhimu kwa wakazi wa Dar es salaam na maendeleo yake ni makubwa hivyo tuwaunge mkono TBA”. Kwa undani zaidi usikose kusoma ripoti ijayo ya utekelezaji wa mradi huu.

Recommended for you