Audio & Video

OSHA kuanzisha Oparesheni Maalum kwa waajiri wote nchini

on

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Wakala wa usalama mahala pa kazi nchini OSHA unatarajia kuanzisha oparesheni maalum kwa waajiri wote ili kuhakikisha ikiwa wamejisajili na wakala huo kama ilivyo matakwa ya kisheria.

Kaimu Mtendaji Mkuu OSHA, Khadija Mwenda ameyasema hayo hii leo kwenye semina/ kikao kazi na wanahabari mkoani Mwanza, kilichofanyika katika ukumbi wa Nyakahoja.

Amesema katika kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi nchini, OSHA imeondoa gharama za ujali kwa kila mwajiri lakini bado mwitikio kwa waajiri kujisajili bado ni mdogo hivyo wakala huo umepanga kuanza oparesheni maalum kuanzia mwezi huu hadi Disemba ili kuhakikisha kila mwajiri anasajiliwa.

Mwenda amesema ikiwa mwajiri atakutwa hajajisajili OSHA hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake hivyo waajiri wote wahakikishe wanasajiliwa kabla oparesheni hiyo haijawafikia kwani kujisajili ni bure.

“Kwa kipindi hiki cha kuanzia mwezi huu Septemba mpaka Disemba, tutaendesha oparesheni maalum katika Kanda zetu sita ambazo ni Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini, Pwani, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kusini na Kanda ya Kati na tutapita kila eneo la kazi kuhakikisha waajiri wamejisajili na kupata cheti cha kukidhi viwango vya usalama”. Amesema Mwenda.

Baadhi ya wanahabari walioshiriki semina/ kikao kazi hicho wameahidi kuitumia vyema elimu waliyoipata kwa kuwaelimisha waajiri na waajiriwa ili kutambua umuhimu wa kuzingatia usalama mahala pa kazi pamoja na kujisajili OSHA.

Takwimu za shirika la kazi duniani ILO zinaonyesha kwamba kila baada ya sekunde 15 mfanyakazi mmoja hupoteza maisha kutokana na ajali ama ugonjwa mahala pa kazi huku wafanyakazi 160 wakipata ajali.

Aidha takwimu hizo zinaonyesha kwamba zaidi ya watu Milioni mbili huumia katika maeneo yao ya kazi kila mwaka na hivyo kusababisha gharama kubwa ikiwemo za matibabu, fidia, ulemavu, vifo na matengenezo ya mitambo sababu kubwa ikiwa ni ukosefu wa usalama mahala pa kazi.

Kaimu Mtendaji Mkuu OSHA, Khadija Mwenda akizungumza kwenye kikao kazi hicho
Mwezeshaji wa semina hiyo, Mjawa Mohamed kutoka OSHA akifafanua jambo
Mwanahabari Mashaka Batazar akichangia mada
Mwanahabari Alex Sanga akichangia mada
Mwanahabari Alex Gwido akichangia mada
Washiriki wakiteta jambo kwenye semina hiyo
Tazama BMG Online Tv hapa chini

Recommended for you