Habari Picha

Wananchi Serengeti watakiwa kuachana na mila zenye madhara

on

Na Frankius Cleophace, Serengeti

Watoto hususani wa kike waliokimbia kuketwa katika wilaya ya Serengeti mkoani Mara wamewaomba wazazi na walezi wao kuachana na mila zenye madhara ikiwemo ukeketaji.

Wamesema mila hizo zinasababisha watoto kuishi nje ya familia zao na hivyo kukosa malezi bora kutoka kwa wazazi na walezi wao hatua ambao husababisha baadhi ya watoto kukosa huduma muhimu ikiwemo elimu.

Hayo yalibainishwa na watoto wa kike wanaolelewa katika Kituo cha Matumaini kwa wasichana na wanawake wilayani Serengeti kwenye tamsha la michezo la kutoa elimu kwa jamii ili kuondokana na mila zenye madhara lililoandaliwa na shirika la RIGHT TO PLAY lililofanyika katika viwanja vya Polisi Mugumu Mjini.

“Baadhi yetu tumetoka familia maskini na wengine tumekimbia kukeketwa na tunaishi kwa mashaka wakati tupo kwenye nchi yetu yenye amanni, kwa nini wazazi wasituhurumie na kuondokana na suala la ukeketaji pamoja na ukatili kwa watoto ili nasi tuishi salama”? Walihoji watoto hao.

Kwa upande wake Titus Mufuruki kutoka dawati la polisi wilayani Serengeti ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo alisema suala la ukeketaji ni kosa kama makosa mengine na kwamba sheria zinamlinda mtoto ikiwemo sheria ya mtoto ya mwaka 2009 hivyo jamii haina budi kuheshimu sheria kwani serikali haitasika kuwachukulia sheria watakaojihusisha na ukeketaji.

Alisema bado kuna ugumu kwa wanajamii kutoa ushahidi kwenye kesi zinazohusu ukeketaji ambapo mwaka 2016 kulikuwa na kesi nane ambapo tatu zilitolewa huku ambapo alitoa rai kwa jamii kutoa ushirikiano pale wanapohitajika.

Naye Leah Kimaro kutoka shirika la RIGHT TO PLAY ambao kwa sasa wanaendelea na matamasha ya kutoa elimu ya kupiga vita mila na desturi zenye madhara ikiwemo ukeketaji alisema kuwa changamoto ya ukeketaji kwa mtoto wa kike wilayani Serengeti inazidi kuzima ndoto za watoto na kuomba jamii kubadilika.

“Sisi kama Shirika tunaendelea kutoa elimu kupitia matamasha haya kwa kutumia mbinu za maigizo, nyimbo, ngonjera na mchezo wa soka kwa wasichana na wavulana ambapo kupitia michezo hiyo tunafikisha elimu ya kuondokana na mila na desturi zenye madhara katika jamii”.  alisema Kimaro.

Mgeni rasmi, Afisa Dawati la Jinsia wilayani Serengeti akizungumza kwenye tamasha hilo

Leah Kimaro kutoka shirika la Right To Play akizungumza kwenye tamasha hilo

Recommended for you