Michezo

Wakenya wang’ara mbio za Rock City Marathon 2017 Jijini Mwanza

on

Naibu Waziri wa Michezo, Sanaa na  Utamaduni, Juliana Shonza (wa pili kulia)  akikimbia  mbio za km 3 katika mashindano ya mbio za Rock City Marathon 2017 yaliyofanyika jijini Mwanza.

Judith Ferdinand, Mwanza

Zaidi ya washiriki 2,000 kutoka ndani na nje ya nchi hii leo wameshiriki mashindano ya mbio za Rock City Marathon 2017 Jijini Mwanza huku Kenya ikiibuka vinara kwenye mbio hizo.

Mbio hizo zinafanyika mara ya nane  mfululizo zikiratibiwa kampuni ya Capital Plus International na kudhaminiwa ambapo wadau mbalimbali ikiwemo Puma, Tiper, NSSF,Red bull, Bodi ya utalii Tanzania, New Mwanza Hotel, EF Out door, CF Hospital, KK Security, CRJE, Dasani, Nyanza Bottler, TRHM na SDS yamejitokeza kudhamini mbio hizo zilizoshirikisha wakimbiaji kutoka Tanzania, Kenya, Japan na Marekani.

Katika mbio hizo zilizofanyika  uwanja wa CCM Kirumba jana  na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu  Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni Juliana Shonza pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ambaye ni Rais wa Chama cha Riadha Tanzania Anthony Mtaka ambao walishiriki mbio za km 3.

Mshindi wa kwanza  wa mbio za km 42 kwa upande wa wanaume ni Abraham Too kutoka nchini Kenya  ambaye alitumia masaa 2 dakika 22 na sekunde 45 , nafasi ya pili alishika Moris Mosima (Kenya)  aliyekimbia masaa 2 dakika 23 na sekunde 18, nafasi ya tatu ilienda kwa Toche Onyango huku wanawake nafasi ya kwanza ilishikwa na Gladys Otero, ya pili Jesca Chibeto na Flavian Kamboka wote kutoka Kenya.

Huku mbio za km 21  upande wa wanawake wa  Kwanza ni Doriphine Omary, wa pili Alice Mugale wote kutoka Kenya na watatu Maselina Issa kutoka Arusha Tanzania, na kwa upande wa wanaume wa kwanza  Peter Limo (Kenya), wapili George Waiyaki (Kenya) na watatu Chacha Boyi kutoka Tanzania.

Pia mashindano hayo yalikua na mbio za km 2.5 maalum kwa watoto ambapo mshindi wa kwanza upande wa wanaume  ni Nuru Leonard, wapili Nelson John na watatu Yohana Masele huku wanawake wa kwanza Sekelo Julius, wapili Mimi Mahenga na watatu Suzan Julius.

Hata hivyo, mashindano hayo yalikua na mbio za km 5 maalumu kwa ajili ya watu wenye ualbino na km 3 kwa wazee, ambapo katika mbio za  km 42 washindi kwa jinsia zote wa kwanza alipata milioni 4 na medali ya dhahabu, wa pili milioni 2 na medali ya siliver na watatu milioni 1 na medali ya shaba, km 21 wa kwanza milioni 2, wa pili milioni 1 na watatu laki tano, huku km 2.5 wa kwanza 150000, wa pili 100000 na watatu 50000 pamoja na medali.

Akizungumzia mashindano hayo mmoja wa washiriki kutoka Kenya  Gladys Otero alisema, mashindano ni mazuri kwani hall ya ulinzi na usalama ilikua nzuri, siri ya wakenya kufanya vizuri ni kutokana na mazoezi mara tatu kwa siku sambamba na kuwa na kambi maalumu kwa ajili ya riadha.

Naye mshiriki kutoka Tanzania  Paschal Mombo alisema, sababu ya kushindwa kufanya vizuri ni kutokana na kukosa mazoezi, hivyo wanajipanga msimu ujao.

Kwa upande wake Naibu Waziri Shonza aliwapongeza waandaaji wa mashindano hayo, ambayo  yanasaidia jamii na taifa kwani yamebeba ujumbe wa kutangaza utalii wa nchi pamoja na kuibuka vipaji vya vijana ambao watawakirisha katika mashindano ya kimataifa na dunia.

Pia alisema, kutokana na mchezo wa riadha kuwa na mwinuko mudogo,ni jukumu la serikali na viongozi wa vyama vya riadha nchini  kushirikiana ili kukuza na kuendeleza mchezo huo, kwa kuwapatia vijana mazoezi,maandalizi ya mapema pamoja na walimu.

Aidha Mtaka aliipongeza Capital Plus International kwa kuandaa mbio hizo ambazo zinashika nafasi ya pili kwa ukubwa nchini,pia imesaidia kuutangaza mkoa wa Mwanza na taifa kwa ujumla.

Vilevile Mkaguzi wa NSSF Mwanza Rashid Gewa ambao ni  moja wa wadhamini wa mbio hizo,alisema mchezo hasa wa riadha ni  afya hivyo wataendelea kuunga mkono ili yaweze kusonga mbele.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo Zenno Ngowi alisema, washiriki nchini wameshindwa kufanya vizuri kutokana na kutokuwa na mazoezi hivyo anaomba wadhamini wawasaidie ili washiriki waweze kukaa kambi na kufanya mazoezi miezi nne kabla ya mashindano.

Recommended for you