Audio & Video

Shule ya wasichana Bwiru yazindua mikakati ya kuongeza ufaulu

on

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Shule ya sekondari ya wasichana Bwiru iliyopo katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, imezindua rasmi mikakati yake ya kielimu inayolenga kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2018/19.

Akitaja mikakati hiyo jana (tazama video hapo chini) kwenye hafla ya kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri zaidi kwenye matokeo ya kidato cha sita yaliyotoka mwezi Mei mwaka huu, Mkuu wa shule hiyo Mwl. Mecktilda Shija alisema lengo ni kuongeza ufaulu kutoka asilimia 99 hadi kufikia asilimia 100.

Mikakati hiyo pia inalenga kuitoa shule hii kongwe hapa nchini kwenye nafasi iliyopo kwani kwa mwaka wa masomo 2016/17 ilishika nafasi ya 24 kati ya shule 25 mkoani Mwanza, nafasi ya 402 kati ya shule 449 kitaifa huku mwaka 2017/18 ikishika nafasi ya 17 kati ya shule 29 kimkoa na nafasi ya 383 kati ya shule 543 kitaifa.

Ili kufikia matokeo bora zaidi, shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI limekuwa likiwajengea uwezo wanafunzi wa shule hii kwa takribani miaka mitatu sasa na matokeo yameanza kuonekana ikiwemo kupambana na suala la ujauzito kwa wanafunzi ambapo uchunguzi uliofanywa mwezi uliopita hakukuwa na mwanafunzi mwenye ujauzito ikilinganishwa na mwaka jana ambapo wanafunzi wawili walibainika kuwa na ujauzito.

Wakati shule hii ikijiwekea mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wanafaulu vyema, wanafunzi nao wanahimiza kuboreshewa mazingira ya wao kujisomea pamoja na utatuzi wa changamoto ya uhaba wa vitabu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Manispaa ya Ilemela ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hii, Afisa Elimu Sekondari Manispaa hiyo Mwl. Emmanuel Malima aliwahimiza wanafunzi kuzingatia masomo kwa mstakabali wa taifa na maisha yao huku akiwasihi kuhakikisha wanaondoa sifuri shuleni hapo.
Afisa Elimu Sekondari Manispaa hiyo Mwl. Emmanuel Malima akizungumza kwenye hafla hiyo

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bwiru, Mwl. Mecktilda Shija (kushoto) akisoma taarifa ya shule hiyo
Mkurugenzi wa shirika la Kivulini, Yassin Ally akifafanua namna shirika hilo limesaidia kuongeza ufaulu katika shule ya sekondari ya wasichana Bwiru
Elizabeth Michael (kushoto) akisoma risala ya wanafunzi
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga akiwasilisha salamu zake kwenye hafla hiyo
Diwani Kata ya Pasiansi, Rosemary Mayunga akiwasilisha salamu zake kwenye hafla hiyo
Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita shule ya wasichana Bwiru wakitunukiwa vyeti vya pongezi baada ya kufaulu kwa wastani wa daraja la kwanza
Mwenyekiti wa Bodi shule ya wasichana Bwiru, Witness Makale (kulia), akipokea zawadi na vyeti kwa niaba ya wahitimu wengine waliopata daraja la kwanza kwenye mtihani wao wa kidato cha sita mwaka huu
Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita shule ya sekondari ya wasichana Bwiru waliofanya vizuri kwenye mtihani wao wa kidato cha sita wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi, uongozi wa shule, Kivulini pamoja na viongozi mbalimbali
Wahitimu nao wakamzawadia Mkuu wao wa shule
Baadhi ya kazi za mikono zinazotengenezwa na wanafunzi wa shule ya wasichana Bwiru
Baadhi ya wahitimu waliopata daraja la kwanza kwenye mtihani wao wa kidato cha sita
Tazama BMG Online Tv hapa chini

Recommended for you