Michezo

WANACHAMA WA SIMBA JIJINI MWANZA WALIVYOADHIMISHA “SIMBA DAY” 2017

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Wanachama na Mashabiki wa klabu ya soka ya Simba Jijini Mwanza, wametoa msaada (zawadi) ya vitu mbalimbali  vyenye thamani ya shilingi 700,000 kwa watoto waliofanyiwa vitendo vya ukatili wanaolelewa na Shirika la Foundation Karibu Tanzania (FKT).

Msaada huo ulitolewa juzi wakati wakisherekeha siku ya  klabu hiyo maarufu kama Simba Day inayoadhimishwa Agousti 08 kila mwaka.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Mratibu wa wanachama hao Philibert Kabago, alisema wameamua kusherekea siku hiyo kwa kuwatembelea watoto hao pamoja na kuwapa zawadi mbalimbali kama biskuti, mafuta ya kupikia, sabuni, unga, sukari na madaftari ili wasione kama jamii imewatenga.

Kabago alisema anasikitika kuona wazazi wanawafanyia ukatili watoto wao hivyo amewaomba wajitambue pamoja na kuchukuliwa hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kuwafanyia ukatili watoto hao.

Naye mmoja wa mashabiki wa klabu hiyo, Arthur Massawe aliziomba klabu mbalimbali za mpira nchini, kutembelea vituo vinavyowalea watoto ili kuwafundisha na kuibua vipaji vya soka kwani wamesahaulika.

Naye Baraka Jackson mmoja wa watoto wanaolelewa na kituo hicho, aliwashukuru wanachama hao kwa msaada walioutoa pamoja na kuitakia kila heri timu ya Simba katika msimu wa ligi kuu unaotarajia kuanza hivi karibuni.

Naye Thereza Geofrey  alisema “Mungu awabariki pamoja na kuwaomba waendelee kuwatembelea  na kuwasaidia”.

Mwakilishi wa FKT, Asunta Ngatunga alisema ni mara ya kwanza mashabiki wa mpira kutembelea kituo hicho tangu kuanzishwa mwaka 2007 hivyo aliwashUkuru wanachama hao huku akiongeza kwamba kwa sasa kituo hicho kina watoto  25 na kwamba tangu kuanzishwa kwake kimewaokoa watoto 286 kutokana na vitendo vya ukatili.

“Watoto hawa wana vipaji mbalimbali hususani vya mpira wa miguu, tatizo wanakabiliwa na ukosefu wa viwanja kwa ajili ya kufanyia mazoezi na kuimarisha vipaji hivyo”. Alidokeza Ngatunga ishara ya kwamba watoto hao wanapaswa kusaidiwa ili kutimiza ndoto zao.

Recommended for you