Habari Picha

Wanafunzi wa chuo cha SAUT waonyesha utayari kuelekea Uchumi wa Viwanda

on

Judith Ferdinand, BMG

Wanachama wa kikundi cha wanafunzi wanawake wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) tawi la Mwanza, wameeleza utayari wao wa kushiriki kwenye dhana ya maendeleo ya kijinsia kuelekea uchumi wa viwanda.

Mwenyekiti wa kikundi hicho, Edina Mwamasangula aliyasema hayo jana katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika chuoni hapo na kuhudhuriwa na Mkuu wa  Mkoa  wa  Mwanza John Mongella ambaye ndiye alikua mgeni rasmi  na kuambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa  Wilaya ya Nyamagana Mary Tesha.

Mwamasangula alisema kikundi hicho kipo tayari kutoa elimu kuhusiana na masuala ya kijinsia mahali popote mkoani hapa na mikoa mingine na kuomba ofisi ya Mkuu wa Mkoa na nyingine zinazoshughulikia masuala hayo katika ngazi ya mkoa na taifa watambue uwepo na utayari wao.

Pia alimuomba Mongella kuwapa fursa ya kushirikishwa na kuwezeshwa katika shughuli mbalimbali za kimkoa na kitaifa hususani vijijini.

“Tunaiomba ofisi yako na ofisi zote zinazoshughulikia  masuala ya kijinsia katika mkoa wetu na kitaifa zitambue kwamba tuko tayari kutoa elimu kuhusiana na masuala hayo, mahali popote hata kushiriki kwenye dhana nzima ya maendeleo ya kijinsia nchini kwetu kupitia chuo chetu cha SAUT, hivyo tunaomba kushirikishwa na kuwezeshwa katika shughuli mbalimbali hususani za vijijini”. Alisema Mwamasangula.

Kwa upande wake Mongella alisema serikali ya awamu ya tano inatoa fursa kwa wanawake na kauli mbiu inazungumzia kusaidia wanawake wa vijijini ambao wanafanya kazi kubwa katika shughuli mbalimbali za uzalishaji ikiwemo kilimo  ambacho watanzania  tunatekitegemea katika maisha na maendeleo ya uchumi wa taifa.

Mongella alisema atashirikiana na umoja huo,pamoja na kuutaka kutengeneza mazingira ya namna   kuwawezesha,kusaidia na kuelimisha jamii hasa wanawake wa  vijijini ili waweze kujitambua.

Sambamba na hayo, aliwataka wanafunzi  wa kike kujikita zaidi katika masomo ya sayansi ili kuendana na teknolojia na kuchochea maendeleo ya taifa .

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Merry Tesha alisema kwa sasa wanawake wa mjini wanajitambua, ni nafasi ya kuhamasisha wa vijijini wajitambue, kwani wanafanya kazi,hivyo wanaume watambue kuwa wa mama hao wanamchango  zaidi katika maendeleo ya uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.

Mmoja wa wanafunzi kutoka shule ya Sekondari ya wasichana Nganza, Jovina Joseph alisema serikali inapaswa kupeleka pembejeo na zana za kilimo kwa wanawake vijijini kwa wakati pamoja na kuanzisha viwanda vidogo katika maeneo yao ili iwe rahisi kupata soko la mazao yao,kwani uwezi kuwa na kiwanda kikubwa bila kuanzia kidogo.

Aidha Afisa Miradi kutoka Shirika la kutetea haki za watoto wafanyakazi wa nyumbani WoteSawa, Cecilia Nyagasi alisema katika kuadhimisha siku hiyo muhimu, shirika hilo limewezesha watoto wafanyakazi wa nyumbani 17 kwa kuwajengea uwezo na kuwapa ujuzi wa mafunzo ya saloon ambapo watatumia kuwasaidia wanawake na watoto wakike vijijini wanakotoka wengi wao.

Vilevile Mshauri wa  kikundi cha wanafunzi wanawake wa  chuo cha SAUT, Joseph Badokufa alisema wataendelea kuleta hamasa na usawa wa kijinsia na kuiomba jamii kuendelea kuwatunza akina mama na kuwapa kile wanachohitaji katika kutimiza ndoto zao na kuishi kwa amani na kumpendeza Mungu.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu inasema ” Kuelekea uchumi wa viwanda, Tuimarishe Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Vijijini” ambapo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka.

Tazama HAPA Maadhimisho ya kimkoa Mwanza.

Recommended for you