Habari Picha

Wanakikundi Mwanza waazimia kujenga hospitali

on

Judith Ferdinand, BMG

Umoja wa Wanakisiwani Wenye Kutafuta Maendeleo (IPDU) mkoani Mwanza umeanza mkakati wa kujenga jengo la ghorofa tano kwa ajili ya hospitali katika eneo la Nyamhongolo Manispaa ya Ilemela litakalolitagharimu  shilingi bilioni tatu.

Mwenyekiti wa umoja huo, Massoud Seif amesema ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kuanza mwezi Novemba mwaka huu ukitarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka 2020 na kurahisha upatikanaji wa huduma za Mama na Mtoto pamoja na matibabu mengine kwa gharama nafuu.

Alisema mpaka sasa wameshapata hati miliki ya eneo hilo na hatua za uchoraji ramani zimekamilika na ipo halmashauri kwa wataalam ili kuweza kuanza na ujenzi huo.

“Tunatarajia jengo hilo litakapo kamilika na kuanza kutoa huduma litalaza wagonjwa zaidi ya 80 na tutapokea kwa siku wagonjwa 100 kutoka sehemu mbalimbali ili kuweza kuokoa wajawazito, watoto na akina mama”. Alisema Seif.

Pia alisema umoja huo wenye wanachama 150 ulianzishwa kwa kwa lengo la kusaidiana katika  shida na raha ila wameamua kwenda mbali zaidi kwa kutoa msaada wa kujenga hospitali ambayo itawasaidia wananchi.

Kwa upande wake Katibu wa IPDU, Aboud Masoud aliwataka wananchi na makampuni mbalimbali kuunga mkono juhudi za serikali kwa kushirikiana nayo katika kuleta maendeleo kwenye maeneo yao.

“Nawaomba wananchi na makampuni mbalimbali ikiwemo vikundi vya maendeleo kuhakikisha wanaungana kwa pamoja ili kusaidiana na serikali katika kufanikisha miradi ya maendeleo namkuwasaidia wananchi wenye uhitaji”. Alisema Masoud.

Recommended for you