Habari Picha

Wananchi Shinyanga wacharuka mbele ya Mkuu wa Wilaya

on

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amefanya ziara ya kusikiliza na kuzitatua kero za wananchi katika kijiji cha Nyaligongo Kata ya Mwakitolyo na Solwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (Shinyanga vijijini).
Mbali na kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi mkuu huyo wa wilaya alizindua zoezi la upandaji miti katika shule ya msingi Manigana iliyopo katika kata ya Solwa kwa kupanda miti ya259 mihare , pamoja na kuzindua ujenzi wa bomba la maji kutoka Ziwa Victoria katika kijiji cha Mwakatola kata ya Solwa.
Ziara ya mkuu huyo wa wilaya iliyofanyika Novemba 8,2017 ilianzia kijiji cha Nyaligongo ambapo alipokea kero mbalimbali zikiwemo za afya ,elimu,ulinzi pamoja na kero kubwa ya wananchi ya kutosomewa mapato na matumizi ambayo ilizua mtafaruku mkubwa kwa wananchi kuwakataa viongozi wao wa kijiji na kutaka waondoke na mkuu wa wilaya wakidai viongozi hao hawafai.
Asilimia kubwa ya wananchi waliohudhuria mkutano huo walikuwa wakiliuliza swali la kutosomewa mapato na matumizi na kudai kuwa viongozi wa kijiji hicho wamekuwa wakizitafuna fedha wanazolipa ushuru na kutofika sehemu husika na hivyo kukwamisha upatikanaji wa maendeleo kwenye kijiji hicho.
Mmoja wa wananchi hao Abdul Saidi alisema kero kubwa ambayo imekuwa ikisumbua kwenye kijiji hicho ni kutosomewa mapato na matumizi kwa muda wa miaka minne sasa, huku viongozi wao wakiendelea kutoza ushuru lakini hawasomi mapato na matumizi na kutokujua akaunti yao ya kijiji mpaka sasa ina shilingi ngapi.
“Mkuu wa wilaya leo tunaomba uondoke na viongozi wote hawa wa kijiji kwa sababu hatuna faida nao ni kikwazo cha maendeleo yetu wanatafuna tu fedha”,alisema Said.
Naye Simoni Kayanda alisema kwenye kijiji hicho kuna plant 30 za kuchenjulia dhahabu na walikubaliana kila mwezi kulipa shilingi 100,000/=  kwa kila Plant kupitia akaunti ya kijiji lakini maendeleo kwenye kijiji hakuna na wala kujua akaunti hiyo inafedha kiasi gani.
Hata hivyo Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Jeremiah Busangija aliposimamishwa na mkuu wa wilaya Josephine Matiro kujibu tuhuma hizo za kutosoma mapato na matumizi alianza kujikanyaga na kutokutoa majibu sahihi wala kutokujua akaunti hiyo ya kijiji ina fedha kiasi gani hali iliyozua taharuki kwenye mkutano huo.
Aidha kufuatia sintofahamu hiyo ilimlazimu mkuu wa wilaya kumuagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo ya Shinyanga Bakari Mosinyo kumpeleka mkaguzi wa hesabu wa ndani  CAG ili kubaini kama kuna ubadhirifu wa fedha kwenye kijiji hicho ili viongozi hao waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Mkuu huyo wa wilaya aliwaeleza wananchi hao kuwa kwa sasa hawezi kuwawajibisha viongozi hao wala kuondoka nao kwani anataka kwanza ajiridhishe kisheria ndipo ajue wapi pa kuanzia.
Matiro alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wote serikali za mitaa wawe na tabia ya kusomea wananchi wao mapato na matumizi kila baada ya miezi mitatu, ili kuondoa manung’uniko ya wananchi kuwa huenda fedha zao ambazo huchanga za maendeleo kuwa zimeshatafuna na wachache.
“Principle ya maendeleo sehemu yoyote ile lazima viongozi wake wawe wawazi,naomba viongozi kuwa wawazi kwani msipokuwa wawazi wananchi hawa hawawezi kuwaelewa,kama tutabaini kuwa kuna ubadhirifu wa fedha lazima wahusika wachukuliwe hatua za kisheria”,alisema Matiro.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya aliagiza Mamlaka ya Uzalishaji na Usambazaji Maji kutoka mradi wa ziwa Victoria KASHWASA ,kumaliza tatizo la maji katika kijiji cha Mahembe ndani ya wiki mbili ili kuwaondolea adha wananchi hao ya kutafuta maji umbali mrefu.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo na Solwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga -Picha na Marco Maduhu – Malunde1 blog
Wananchi wa kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo wakiwa kwenye mkutano wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akitatua kero zao
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi
Wakazi wa kijiji wa Nyaligongo wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro
Mmoja wa wafanyabiashara wa uchenjuaji dhahabu Sultan Simon akimweleza Mkuu wa wilaya jinsi viongozi wa kijiji cha Nyaligongo wanavyofanya ubadhirifu wa fedha ambapo alisema mwezi uliopita amelipa Shilingi laki moja kwenye akaunti ya kijiji kupitia Benki ya NMB na hivyo akaeleza alisikitishwa na mwenyekiti wa kijiji  kudai kuwa hajui kuna pesa kiasi gani kwenye akaunti ya kijiji
Mwananchi Simon Kayanda ,amewasilisha kero ya kutaka kusomewa Mapato na Matumizi na kuutuhumu uongozi wa kijiji kutafuna fedha na wakati kijijini hapo wana Plant 30 za kuchenjulia dhahabu na walikubaliana kila Plant ilipe shilingi 100,000 kila mwezi, pamoja na kodi zingine shilingi 50,000 ,lakini kijiji hicho hakina maji, na barabara zake ni mbovu na hawajui pesa ambazo wanazitoa hupelekwa kwenye matumizi yapi.
Mtendaji wa Kijiji cha Nyaligongo Jeremiah Busangija, akijieleza kwa wananchi kuwa akaunti ya kijiji ina shilingi ngapi ambapo alijikanyaga na kudai hajui ,huku akijitetea kuwa mwezi Juni mwaka huu alisomea wananchi wake mapato na matumizi, na hali iliyomlazimu mkuu wa wilaya Josephine Matiro kuagiza uongozi mzima wa kijiji hicho uchunguzwe na mkaguzi wa fedha za ndani CAG pamoja na TAKURURU
Wananchi wakiwa katika mkutano
Mwananchi Elias Amos akiwasilisha kero kwa Mkuu wa wilaya ,kuwa Shule ya Msingi katika kijiji hicho cha Nyaligongo haina vyoo na viongozi wao wamekuwa wakitafuna fedha za michango na hivyo kurudisha maendeleo nyuma.
Elias Amos akieleza kero yake kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro
Abduli Said akiwasilisha kero kwenye mkutano wa mkuu wa wilaya Josephine Matiro ambapo alidai kijiji cha Nyaligongo hakina ulinzi ,mazingira ni machafu na hawasomewi mapato na matumizi.
Sabatia Amos wachimbaji wadogo wa Dhahabu akieleza kuwa kijiji cha Nyaligongo wanakabiliwa na tatizo la ulinzi kwani hakuna kituo cha polisi na kusababisha watu kufa hovyo na kuiomba serikali ipeleke kituo cha polisi kijijini humo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.

 

Wananchi wakiwa katika mkutano huo
Mkurugenzi wa halmashauri ya Shinyanga Bakari Kasinyo akizungumza katika mkutano huo ambapo aliwataka wanakijiji hao ambao shughuli yao kubwa ni uchimbaji wa madini ya dhahabu, kulipa kodi za serikali kwa mujibu wa sheria kwa kufuata sheria ndogo ambazo zimeshapitishwa na madiwani wa halmashauri hiyo.
Diwani wa kata ya Mwakitolyo Limbe Agustino akizungumza katika mkutano huo ambapo alisema kero zingine za wananchi wa kata hiyo zipo kwenye ufumbuzi na kinachotakiwa sasa ni kusubiri ni utekelezaji ,ikiwa suala la umeme lipo kwenye mpango wa umeme wa REA, huku zahanati ramani yake ipo ,pamoja na tatizo la maji litatuliwa muda si mrefu
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mahembe kata ya Mwakitolyo ambapo pia alikutana na kero ya maji ambayo hapo awali yalikuwa yakitoka lakini tangu mwezi Julai mwaka huu maji hayo hayakutoka tena ,na hivyo kuagiza uongozi wa KASHWASA kulimaliza tatizo hilo ndani ya wiki mbili.
Wananchi wa kijiji cha Mahembe wakimsikilza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akitatua kero zao ikiwemo ya  elimu, afya ,kilimo na maji.
Mmoja wa wananchi wa kijiji  cha Mahembe Shija Ruzumba akizungumza katika mkutano huo ambapo alisema tatizo la maji kutotoka kwenye kijiji hicho lilisababishwa na kitendo cha kufukuzwa kwa mmoja wa wasimamizi wa mradi wa maji kwenye tanki la kijiji hicho na tangu afukuzwe maji yalishagoma kutoka hadi leo
 Kaimu mkurugenzi wa KASHWASA ,Laurence Wasara akizungumza katika mkutano huo ambapo alikiri maji katika eneo hilo kugoma kutoka tangu mwezi  Julai 2017 na kudai wametafuta tatizo lakini wameshindwa na hivyo kuhofia huenda kuna ushirikina ,huku akimuahidi mkuu huyo wa wilaya kujaribu kulitatua tatizo hilo ndani ya wiki hizo mbili na ikishindikana itabidi yafanyike maombi maalum.
Akina mama wakiwa katika mkutano huo
Tunatatuliwa kero zetu…
Wananchi wakiwa katika mkutano
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akipanda mti katika shule ya msingi Manigana kata ya Solwa ,ambapo imepandwa miti 258 ya mihare.
Mkuu wa wilaya akichimba mtaro wa kupitisha bomba la maji katika kijiji cha Mwakatola ,ambalo litakamilika mwishoni mwa Novemba Mwaka huu.
Mkuu wa wilaya akichimba mtaro wa kupitisha bomba la maji katika kijiji cha Mwakatola ,ambalo litakamilika Mwishoni mwa Novemba Mwaka huu.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Bakari Kasinyo na Ofisa tawala wa wilaya ya Shinyanga Charles Maugira wakisaidizana na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro kuchimba mtaro wa bomba la maji
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akichimba mtaro
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwapongeza wananchi kwa kujitolea kuchimba mtaro huo wa maji ,ikiwa maendeleo huletwa na wananchi wenyewe.
Picha zote na Marco Maduhu – Malunde1 blog

Recommended for you