Audio & Video

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA yasisitiza Maudhui yanayopaswa

on

George Binagi-GB Pazzo

Mamlaka ya Mawasilino Tanzania kupitia Kamati yake ya Maudhui jana imetoa semina kwa Wahariri, Watangazaji na Wataarishaji wa Vipindi vya Luninga na Redio Kanda ya Ziwa, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kuandaa na kutangaza habari, vipindi na makala zinazozingatia maadili katika jamii.

Katika mada ya kwanza iliyohusu Maudhui ya Kitamaduni iliyowasilishwa na Derrick Murusuri kutoka Kamati ya Maudhui TCRA, wanahabari walihimizwa kutumia vyombo vya habari katika kujenga dhana na imani aminifu katika jamii kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

“Vyombo vya habari vina nguvu kubwa ya kujenga dhana ama imani aminifu katika jamii, hivyo tuanze kwa kubadilika sisi wanahabari kwa kulifahamu vyema jambo kabla ya kulipeleka katika jamii. Tusijikite sana kwenye vile vipindi vya kigeni kwani vinatubadilisha na kutuharibu na hivyo kutufanya waafirika kujiona wanyonge mbele ya wageni (weupe)”. Alisisitiza Murususi.

Mada ya kuhusu Maudhui yanayolenga Maendeleo iliyowasilishwa na Joseph Mapunda ambaye ni Makamu Mwenyekiti Kamati ya Maudhui TCRA, iliwakumbusha zaidi wahariri na waandaaji hao wa vipindi  kutumia vyombo vya habari kujenga misingi imara ya kimaendeleo katika jamii kwa kutoa habari zinazochochea zaidi maendeleo ya taifa.

“Hata hivyo pamoja na wingi wa vyombo vya habari na utangazaji hapa nchini, bado habari nyingi zinahusu matukio yanayowalenga wachache na kuupamba umaskini badala ya kusikia vikitangaza maendelo ya Tanzania na Afrika kwani wakati wote hujilegeza kwenye matatizo na umaskini na kuainisha umma kwamba sisi  ni maskini na wenye matatizo wakati wote, na vyombo hivyo hivyo utakuta vikitoa fursa kwa vyombo vya nje kutangaza habari zao”. Alisema Mapunda.

Alisema lazima vyombo vya habari Tanzania vibadilike na kupamba juhudi za maendeleo ikiwemo namna taifa limedhamiria kusonga mbele kimaendeleo ili kuhakikisha kunakuwa na uwiano mzuri kati ya taarifa na maendeleo ya waanchi wakati ambapo taifa linaelekea kwenye uchumi wa kati kupitia viwanda.

“Vyombo vya habari lazima vitoe kipaumbele kwenye maendeleo ya taifa ikiwemo uchumi wa viwanda, sekta muhimu za kitaifa kama Kilimo na utalii kwani vimepewa dhamana kubwa katika kuleta maendeleo”. Alidokeza Mapunda

Katika mada ya tatu kuhusu Misingi Bora ya Utangazaji iliyowasilishwa na Abdul Ngarawa kutoka Kamati ya Maudhui TCRA, waandaaji wa vipindi na watangazaji waliaswa kusoma na kujifunza kila wakati mambo muhimu ya kitaifa ikiwemo kuelewa vyema masuala ya nchi kama vile Katiba, mwelekeo wa kisiasa, uchumi, sheria na mengineyo.

“Ni muhimu mtangazaji akaendelea kujifunza na kujenga urafiki na watu wanaomzunguka ili aendelee kupata taarifa muhimu na asijenge visasi kwa watu wengine. Lazima awe mahili wa matamshi ili yasimuumize msikilizaji. Mtangazaji anapaswa kuisoma habari kwa urahisi ili eleweke kwa msikilizaji”. Alisema na kuongeza;

“Ni vyema kuwa na maandalizi ya mapema ili kukamilisha vipindi vyako, kufuata na kuzingatia maadili ni muhimu kwa mtangazaji. Pia usitumie utangazaji kama njia ya kuvuka kwenda kwenye sekta nyingine, ukianza kwenye sekta hii baki huku huku”. Ngarawa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui TCRA, Valerie Msoka pamoja na Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandizi Lawi Odiero waliwahimiza waandaaji wa vipindi, watangazaji na wahariri kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utangazaji kwani siku za hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikikiuka mambo hayo na kwamba TCRA itaendelea kusimamia taratibu zilizopo.

Baada ya mada hizo kuwasilishwa, ulifuatia wasaa wa maswali kutoka kwa washiriki na hapa BMG Habari #PamojaDaima inakuletea kwa ufupi maswali na majibu kutoka kwenye warsha hiyo iliyofanyika Jijini Mwanza.

Washiriki wa warsha hiyo wakiwemo wahariri, watangazaji, waandaaji wa vipindi na wasikilizaji/ watangazaji.

Bonyeza BMG Habari, Pamoja Daima kutazama video zaidi

Recommended for you