Audio & Video

WATOTO 25 WAPATA MIKATABA AJIRA JIJINI MWANZA

on

Na George Binagi-GBPazzo

Shirika la kutetea haki za watoto wafanyakazi wa nyumbani nchini WOTESAWA, limewasaidia takribani watoto 25 ambao ni wafanyakazi wa majumbani Jijini Mwanza kupata mikataba yao ya kazi.

Hatua hiyo kubwa kimafanikio katika sekta ya ajira kwa watoto wafanyakazi wa majunyumbani imefikiwa baada ya shirika hilo kutoa mafunzo kwa waajiri na waajiriwa kuhusu umuhimu wa mkataba wa kazi kwa mtoto mfanyakazi wa nyumbani.

Itakumbuka kwamba mtoto mfanyakazi wa nyumbani analindwa na sheria kadhaa ikiwemo sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009, sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2017, waraka wa mishahara wa mwaka 2013 pamoja na katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mratibu wa shirika la WOTESAWA, Cecilia Nyangasi amesema lengo ni kuwajengea uelewa waajiri na waajiriwa ili kuwajengea mahusiano mema waajiri na waajiriwa katika kazi ili kila upande utimize wajibu wake ambapo hatua hiyo itasaidia kuondoa vitendo vya ukatili na unyanyasanyi kwa watoto wafanyakazi wa nyumbani.

Naye Afisa Kazi kutoka Idara ya Kazi mkoani Mwanza, Mohamed Majaliwa amewatahadharisha waajiri ambao wamekuwa wakikiuka sheria zinazowalinda watoto wafanyakazi wa majumbani na kuwasihi kufika ofisi za Idara ya Kazi ili kuelimishwa zaidi kabla ya kuingia kwenye makubaliano ya ajira kwenye sekta ya majumbani hatua ambayo itasaidia kupunguza migogoro katika sekta hiyo.

Waraka wa mishahara wa mwaka 2013 unaelekeza kwamba mfanyakazi wa kazi za nyumbani anapaswa kulipwa kiwango cha chini cha mshahara ambacho ni shingili 150,000 iwapo mwajiri ni balozi ama mfanyabiashara mkubwa, elfu 80,000 ikiwa mwajiriwa haishi kwenye nyumba ya mwajiri wake, elfu 40,000 ikiwa mwajiriwa anaishi kwenye nyumba ya mwajiri wake na shilingi 130,000 ikiwa mwajiri ni rai wakigeni.

Afisa Kazi mkoani Mwanza, Mohamed Majaliwa akitoa mafunzo kwa waajiri na waajiriwa wa sekta ya majumbani

Mafunzo haya yatasaidia waajiri na waajiriwa kusaini mikataba ya ajira, kuongeza hadhi na thamani ya kazi kwa watoto wafanyakazi wa nyumbani na pia kupunguza vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa watoto hao.

Afisa Miradi kutoka Shirika la WOTESAWA, Simon Lucas akitoa mwongozo kwenye semina hiyo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ambao ni waajiri na waajiriwa katika sekta ya ajira za majumbani.

TAZAMA ZOEZI LA KUSAINI MIKATABA HIYO.

TAZAMA VIDEO HAPO CHINI

Recommended for you