Habari Picha

Wazee Jijini Mwanza waigeukia Serikali

on

Picha kutoka maktaba

Juddith Ferdinand, Mwanza

UMOJA  wa  Wazee  Kata ya Kirumba (UWAZEKI) uliopo wilayani Ilemela mkoani  Mwanza, umesema  serikali  imekuwa haiwashirikishi kwenye miradi ya maendeleo inayotolewa katika maeneo yao zikiwemo tenda mbalimbali  ambazo huwabagua na kuwapa kipaumbele vijana na akina mama.

Malalamiko ya wazee hao yalibainishwa wakati wakizungumza ofisini kwao  mtaa wa Ngara katani hapo, ambapo walizungumzia changamoto mbalimbali wanazokutanazano huku wakiiomba serikali  kuboresha dirisha la wazee  ili wapate huduma stahiki.

Mwenyekiti wa Umoja huo Deodatus Mtamizi,  akizungumza  kwa niaba ya wazee hao  alisema  ni vema serikali kuweka uratatibu wa kuwapatia fedha kama asilimia 10  wanavyopatiwa vijana na wakinamama zinazotokana na   mapato yanayokusanywa na halmashauri, ili  nao waweze kujikwamua kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi.

“Tunaomba serikali  itushirikishe  na sisi katika  miradi ya  maendeleo  inayotolewa katika  maeneo yetu  kwa mfano tenda mbalimbali   ambazo zinatolewa  kwani hushirikisha vijana   na akina mama  lakini wazee  tunawekwa  pembeni  kitendo ambacho siyo kizuri,”alisema Mtamizi.

Hata hivyo  aliendelea kuiomba serikali  kuwajali , kuwathamini  na kuwafikiria  wazee kwa kuwakatia bima ya afya  kwani  hawana uwezo wa  kukata kutoka na  kukosa fedha na uchumi kuyumba.

“Wazee  wengi tunategemea kupewa fedha na  watoto wetu,  wajukuu na wasamalia wema   kutokana na hali ya uchumi kuwa ngumu,  imekuwa  tatizo kwani wengi  hufia ndani kwa kushindwa kwenda hospitali  kwa kukosa fedha,alisema Mtamizi.

Vilevile alisema, wazee ni dhahabu ya kijani ni vema kuwathamini kwa kuwa karibu nao ili kuweza kutambua  kero zao zinazowakabili  na kuzitatua.

Aidha waliomba viongozi kuweka utaratibu  wa kuwatembelea katika vyama vyao,  ili kutambua kero  zinazowakabili  sambamba na kupata ushauri  kutoka kwao katika kuendesha nchi hii, kwani wanajua mambo mengi ambayo yatasaidia kuleta maendeleo  na kukuza uchumi wa viwanda.

“Ikumbukwe kuwa wazee tupo na tulikuwepo na tutaendelea kuwepo ni lazima  watambue umuhimu wetu,”alisema Mtamizi.

Recommended for you