Audio & Video

Biteko aonya ukwepaji kodi katika machimbo ya Kaolin wilayani Kisarawe

on

Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko (kushoto) akizungumza na mmoja wa wanunuzi wa madini ya Kaolin, Andy He (kulia) kutoka kampuni ya Keda baada ya kutembelea machimbo/ migodi ya madini hayo katika wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko amefanya ziara ya kutembelea migodi ya madini ya Kaolini katika wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani na kuwahimiza wawekezaji katika migodi hiyo kuhakikisha wanalipa kodi stahiki za serikali.

Biteko alifanya ziara hiyo jana na kukagua shughuli za uchimbaji madini katika migodi ya RAK Kaolin Mining uliopo Kijiji cha Kimani pamoja na Abbeys katika Kijiji cha Dalu na kusisitiza wawekezaji katika migodi hiyo kulipa kodi ya mrabaha kutokana na bei ya kuuzia kiwandani na si bei ya mgodini.

“Sisi hiyo tunaona ni kama utorokaji wa kodi na tumewasisitiza wachimbaji wetu wote wazingatie sheria, walipe kwa kufuata bei wanayouzia kwenye kiwanda (Grose Value) na kwa sehemu kubwa wamefanya hivyo kwenye migodi yote tuliyoitembelea”. Alisema Biteko.

Aidha Biteko alisisitiza kwamba sheria ya madini na kanuni zake za mwaka 2018, inasisitiza kila mwenye leseni ya uchimbaji madini kutunza kumbukumbu za uzalishaji wake mgodini na kwamba anayeshindwa kufanya hivyo adhabu yake ni faini kuanzia shilingi Milioni 50 hadi 150 hivyo wenye migodi wahakikishe wanatunza taarifa zao muhimu ikiwemo za uchimbaji na mauzo.

Katibu Tawala wilayani Kisarawe, Mtela Mwampamba alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wilayani humo na kwamba serikali itaendelea kuwasimamia vyema kwa mujibu wa sheria huku akibainisha kuwa changamoto za ulipaji fidia katika maeneo ya wananchi zimetatuliwa kwa zaidi ya asilimia 90.

Mmoja wa wawekezaji, Haji Nyambi ambaye ni Meneja Mgodi kutoka kampuni ya Abbeys Construction inayochimba mchanga/ madini ya Kaolin katika Kijiji cha Dalu, aliomba Halmashauri ya Kisarawe kujenga mizani ya kupima uzito wa magari ya kubeba madini hayo tofauti na sasa ambapo wanalipa ushuru kwa kukadiria na hivyo bei kubwa tofauti na mzigo halisi. Madini ya Kaolin hutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali za ujenzi ikiwemo “Gypsum”.

Recommended for you