Audio & Video

DHANA POTOFU KWENYE UCHANGIAJI DAMU.

on

Benki ya damu salama Kanda ya Ziwa imesema baadhi ya changamoto zinazosababisha upungufu wa damu katika benki hiyo ni pamoja na imani potofu kwa baadhi ya wananchi ambao huamini wakichangia damu watapata madhara ya kiafya, jambo ambalo si sahihi.

Aidha benki hiyo pia imebaini kwamba hofu ya baadhi ya wananchi kupimwa virusi vya ukimwi husababisha wasite kujitokeza kuchangia damu ambapo imetumia fursa hii kuwasihi kuondoa dhana hiyo kwani ni mapenzi ya mchangia damu kuhitaji majibu ya usalama wa damu yake ama laa, huku viongozi wa taasisi mbalimbali ikiwemo za kidini na elimu wakitakiwa kuwajengea wananchi hamasa ya kuchangia damu mara kwa mara.

Afisa Mhamasishaji wa damu kutoka benki hiyo, Bernadino Medaa, ameyasema hayo wakati akizungumza na Lake Fm Mwanza katika kuelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya kuchangia damu duniani mwaka huu.

Medaa amewahimiza wananchi wote kujenga desturi ya kuchangia damu mara kwa mara ili kufikia chupa laki tatu zinazokidhi mahitaji kitaifa ambapo mwitikio wa wananchi kuchangiaji damu kwa sasa bado uko chini ya asilimia 50 hatua ambayo inahatarisha maisha ya wahitaji wa damu ikizingatiwa hakuna kiwanda cha damu isipokuwa kila mwananchi kuchangia damu hiyo.

Kilele cha maadhimisho ya siku ya kuchangia damu duniani yatafanyika kesho juni 14 ambapo kwa mkoa wa Mwanza yatafanyika katika ofisi za benki ya damu Bugando Jijini Mwanza, lengo likiwa ni kutambua mchango wa wachangiaji damu kote duniani, ikizingatiwa kuchangia damu ni dhawabu kubwa katika maisha ya mwanadamu, kama alivyosisitiza pia Medaa. Tazama video hapa chini.

Recommended for you