Habari Picha

RAIS MAGUFULI ASIKITISHWA NA RIPOTI YA PILI YA MAKINIKIA.

on

Profesa Nehemiah Osoro leo Juni 12,2017 amemkabidhi Rais Magufuli ripoti ya pili ya uchunguzi wa madini yaliyo kwenye makontena 227  ya mchanga wa madini yaliyozuiliwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Ripoti hiyo kama ilivyokuwa ripoti ya kamati ya kwanza, imebaini udanganyifu mkubwa kuhusiana na makotena ya mchanga wa dhahabu (makinikia) yaliyokuwa yakisafirishwa kwenda nje ya nchi, kwa minajiri ya kwenda kuchenjuliwa.

Profesa Osoro amebainisha kwamba serikali imepata hasara ya shilingi Tirioni 108 kutokana na ukwepaji wa kodi uliofanywa na makampuni mbalimbali ya madini tangu mwaka 1998 hadi mwaka huu 2017.

Rais Magufuli amesikitishwa na yaliyokuwa yakiendelea kuhusiana na usafirishaji huo, akisema watanzania walikuwa wakiibiwa mno huku kukiwa na viongozi ambao walikuwa hawafuatilii kujua undani wa makinikia hayo.

Rais Magufuli ameyakubali mapendekezo yote ya kamati hiyo na ameagiza vyombo vya dola kuwachunguza wote waliotajwa kwenye ripoti hiyo, wakiwemo mbunge wa Bariadi Magharibi Endrew Chenge na mbunge wa Sengerema William Ngeleja kwa kuhusika na mikataba ya madini iliyosainiwa miaka iliyopita.

Kamati hiyo ya pili pia imewataka aliyekuwa mbunge wa Handeni marehemu Dkt.Abdallah Kigoma pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona kuhusika na mikataba iliyoliibia taifa.

Aidha usajili wa kampuni ya Acacia umeonekana kuwa wa utata na kubainika haina uhalali wa kufanya kazi nchini hivyo Rais Magufuli ameagiza wizara zinazohusika ziwaite viongozi wa kampuni hiyo kwa ajili ya majadiliano ili iilipe serikali hasara iliyopatikana kabla ya kuanza kushughulikia usajili wake.

Rais Magufuli ameagiza sheria zote za madini zirudishwe bungeni ili zifanyiwe marekebisho kwani zimekuwa zikidaiwa kuliibia taifa kwa kisingizio cha wawekezaji. Amesikitishwa namna taifa lilivyokuwa likiibiwa huku mahospitalini kukiwa hakuna madawa pamoja na huduma nyingine muhimu.

                                                     Mwenyekiti wa Kamati ya pili ya Makinikia

                                                      Viongozi mbalimbali Ikulu Jijini Dar es salaam