Michezo

WANAHABARI WASOMESHWA NAMBA RAMADHANI CUP JIJINI MWANZA.

on

Judith Ferdinand, Mwanza

Waandishi mkoani Mwanza, wamehimizwa kuungana pamoja ili kuhakikisha timu ya Wanahabari  inashinda katika mchezo wao uliosalia katika ligi ya Ramadhani, inayoendelea kutimua vumbi kwenye uwanja wa Mirongo jijini Mwanza.

Wito huo ulitolewa jumamosi na nahodha wa timu hiyo, Moses Wiliam baada ya kumalizika kwa mchezo wao uliowakutanisha na Mbugani FC.

Katika mchezo huo, timu ya Wanahabari  ilijikuta ikishindwa kufurukuta dhidi ya wapinzani wao Mbugani FC baada ya kufungwa goli 3-0, kipindi cha pili ambapo magoli yote yalifungwa na Boniface Elias.

“Mechi ilikua nzuri ila wapinzani wetu walituzidi nguvu kipindi cha pili, hivyo wito kwa wanahabari  ni tuungane pamoja kwani tumebakiza mechi moja ya tarehe 20 juni ambapo tukishinda itatusaidia kufuzu kuingia robo fainali,” Alisema William.

Mchezaji wa Mbugani FC, Boniface Elias alisema mchezo umekua mzuri kwa upande wao na kuibuka na ushindi kutokana na kuzingatia mafunzo waliyopewa na kocha wao na lengo lao ni kuwa mabingwa wa ligi hiyo msimu wa 2017.

Naye  Mkurugenzi wa Ramadhani cup , Shafii Said  maarufu  (Chaku), alisema lengo  la kuanzisha ligi hiyo ni  kuwaepusha vijana katika makundi mabaya hasa katika kipindi hiki cha  mwezi wa Ramadhani pamoja na  kukuza na kuendeleza vipaji.

Pia alisema kumekua na changamoto ya ukosefu wa waamuzi,hivyo kuomba chama cha waamuzi mkoa kuwasaidia sambamba na wadau wengine kujitokeza kudhamini ligi hiyo,ili kuibua vipaji na kuendeleza mchezo wa soka nchini.

Recommended for you